PROFESA MBARAWA:SERIKALI HAITAKI TAFITI ZINAZOISHIA KWENYE MAKABRASHA

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WAZIRI wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amewataka watafiti nchini kuhakikisha tafiti wanazofanya katika sekta ya usafiri na usafirishaji zinatoa suluhisho la changamoto halisi, badala ya kuishia kwenye makabrasha na mikutano.

Akizungumza leo Agosti 20, 2026  wakati akifungua mkutano wa kimataifa unaohusu usafiri, lojistiki na usimamizi, kuwa mafanikio ya utafiti yanapaswa kupimwa kwa matokeo yanayoonekana katika maisha ya wananchi na uchumi wa nchi.

Alisema tafiti  zinapaswa kusaidia Serikali kupunguza gharama za usafirishaji na usafirishaji wa mizigo, kuongeza ufanisi wa bandari na reli, kuboresha usalama wa usafiri pamoja na kujenga miundombinu inayoweza kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Tanzania haihitaji tafiti zinazoishia katika kuandaa taarifa na kuhifadhiwa kwenye makabrasha. Tunahitaji tafiti zinazobadilisha maarifa kuwa vitendo na kuleta matokeo yanayopimika,” alisema Profesa Mbarawa.

Alisema serikali inahitaji tafiti zitakazosaidia kupunguza gharama za usafirishaji na lojistiki, kuongeza ufanisi wa bandari na reli, kuharakisha usafirishaji wa abiria na mizigo na hatimaye kuifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha usafiri, lojistiki na biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini.

Profesa Mbarawa alisema sekta ya usafiri siyo suala la kuhamisha watu na mizigo pekee, bali ni kichocheo cha biashara, uwekezaji, uzalishaji na ukuaji wa uchumi.

Alisema serikali inaendelea kuwekeza katika miundombinu mbalimbali ya usafiri, ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), kuboresha bandari, kuimarisha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), kupanua mfumo wa mabasi yaendayo haraka (BRT), kuboresha barabara na kuendeleza usafiri wa majini.

Aidha alibainisha kuwa  ujenzi wa miundombinu pekee hautoshi bila kuhakikisha inafanya kazi kwa ufanisi na kuunganisha mifumo mbalimbali ya usafiri.

“Tunataka kujenga mfumo mmoja wa usafiri uliounganishwa ambapo reli, barabara, bandari, viwanja vya ndege na usafiri wa majini vinafanya kazi kwa ufanisi,” alisema.

“Mfumo huo utasaidia kupunguza gharama za usafirishaji, muda wa mizigo kufika sokoni na kuongeza usalama pamoja na kuboresha huduma kwa wananchi.

Profesa Mbarawa alisema miundombinu ya usafiri inapaswa kutazamwa kama fursa ya kiuchumi kwa wananchi, kwa kuwa lengo la Serikali si kujenga miundombinu pekee bali kuhakikisha inazalisha fursa za biashara, ajira na uwekezaji.

Alisema mabadiliko ya teknolojia, ikiwemo teknolojia za kidijitali na akili mnemba, pamoja na mabadiliko ya tabianchi, yanaendelea kubadilisha namna mifumo ya usafiri inavyopangwa na kuendeshwa.

Kutokana na hali hiyo, alisema watafiti wanapaswa kutoa mapendekezo yanayoweza kutekelezwa na ambayo matokeo yake yanaweza kupimika.

“Sitaki uchumi ukuwe halafu usafiri ufuate; usafiri wenyewe lazima uwe kichocheo cha ukuaji wa uchumi nchini,” amesema.

Aidha, alisema tafiti zinapaswa kusaidia Serikali kujenga miundombinu inayoweza kuhimili changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.

Alisema mafanikio ya mkutano huo hayapaswi kupimwa kwa idadi ya washiriki, muda wa mkutano au mada zitakazowasilishwa, bali kwa suluhisho zitakazopatikana na sera zitakazoboreshwa kutokana na matokeo ya tafiti.

“Natoa wito kwa watafiti kutumia mkutano huu kuleta mapendekezo yanayotekelezeka na yenye matokeo yanayopimika,” alisema Profesa Mbarawa.

Aliongeza kuwa Serikali iko tayari kushirikiana na watafiti katika kuhakikisha maarifa yanayotokana na tafiti yanatumika kutatua changamoto za usafiri na usafirishaji nchini.

Profesa Mbarawa alisema usafiri wenye ufanisi ni muhimu katika kujenga uchumi wenye ushindani, kukuza viwanda, biashara na kuimarisha uhusiano wa Tanzania na masoko ya kikanda na kimataifa.

Aliwataka washiriki wa mkutano huo kushirikiana na Serikali kujenga mfumo wa usafiri ulio salama, wenye ufanisi, uliounganishwa na wenye ushindani, unaosafirisha watu na mizigo kwa gharama nafuu na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Akimkaribisha mgeni rasmi Mkuu  wa Chuo Cha Usafirishaji (NIT) Dk.Prosper Mgaya alisema kongamano la mwaka huu linajadili mada kuu inayolenga usafiri janja, endelevu na wenye muunganiko kwa ajili ya kurahisisha usafirishaji na biashara, ikiwemo matumizi ya teknolojia katika kuboresha sekta hiyo.

Alisema Tanzania inahitaji mfumo wa usafirishaji unaounganisha reli, barabara, anga na usafiri wa majini ili kurahisisha usafirishaji wa watu na mizigo ndani na nje ya nchi.

Alitoa mfano wa miundombinu ya usafiri wa majini Kigoma, akisema mizigo inayosafirishwa kwa reli inaweza kuunganishwa na usafiri wa majini kuelekea nchi jirani za Burundi na Rwanda.

“Tunatamani usafiri uwe janja, unaotumia teknolojia na unaozingatia mazingira. Pia tunatamani uwe na muunganiko, kwa sababu sasa tuna reli, usafiri wa anga na majini,” alisema.

Alisema pamoja na Serikali kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji, bado kuna umuhimu wa kuwa na usimamizi na maamuzi sahihi ili miundombinu hiyo itumike kwa ufanisi.

Alisema kongamano hilo linatoa fursa kwa wataalamu, Serikali na sekta binafsi kujadili changamoto zinazokabili sekta ya usafirishaji na kutafuta suluhisho ambazo zinaweza kutekelezwa kwa vitendo.

“Tunapowasiliana na kujadili changamoto hizi, tunatarajia kupata majibu ambayo Serikali na sekta binafsi wanaweza kuyatumia katika kuhakikisha changamoto za sekta ya usafirishaji zinapatiwa ufumbuzi,” alisema.

Aidha, aliishukuru Wizara ya Uchukuzi na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, kwa kuendelea kuunga mkono kongamano hilo tangu lilipoanzishwa.