UJENZI WA MELI MPYA NA CHELEZO KIGOMA KUFUNGUA SOKO LA BIASHARA KIMATAIFA- WAZIRI MBARAWA

Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema uwekezaji wa kampuni ya kizawa ya Dar es Salaam Merchant Group katika ujenzi wa chelezo na meli mpya mkoani Kigoma utaongeza uwezo wa Tanzania kujenga na kukarabati meli nchini, huku ukifungua fursa za biashara na huduma za ujenzi wa meli kwa nchi zinazozunguka Ziwa Tanganyika, ikiwemo DRC na Zambia

Prof. Mbarawa ameyasema hayo baada ya kukagua eneo la Bulombora Mkoani Kigoma linalojengwa chelezo cha kampuni hiyo, akisema Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kushiriki katika uwekezaji wa miundombinu na huduma za usafiri wa njia ya maji hatua ambayo itaongeza uwezo wa wazawa katika ujenzi na ukarabati wa vyombo vinavyosafiri kwa njia ya maji.

Amesema kampuni hiyo, iliyoshiriki katika ujenzi na ukarabati wa meli ikiwemo MV Liemba, imeanza maandalizi ya ujenzi wa meli mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 400 za mizigo, Meli ambayo itaongeza uwezo wa usafirishaji katika Ziwa Tanganyika na kuchochea biashara kati ya Kigoma, Katavi, Rukwa na nchi jirani

Prof. Mbarawa amesema mradi huo unaendana na azma ya Serikali ya kuwawezesha wazawa kushiriki katika miradi mikubwa ya maendeleo na kuongeza uwezo wa ndani katika sekta ya uchukuzi, akiahidi Serikali kuendelea kutoa ushirikiano ili mradi ukamilike kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Dar es Salaam Merchant Group, Bw. Rayton Kwembe, amesema sehemu ya kwanza ya chelezo inatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, huku maandalizi ya ujenzi wa meli mpya yakiendelea

Eneo hilo, lililopo kilomita 25 kutoka Kigoma mjini, lina ukubwa wa mita za mraba 95,000 na litakuwa na maeneo ya kutengeneza na kuunganisha vitalu vya meli, kujengea meli pamoja na floating dock kwa ajili ya kuingiza na kushusha meli kwenye maji.

Aidha, kampuni hiyo imesema imeanza kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini katika ujenzi wa meli, ikiwemo viti, makabati, vitanda na samani nyingine. Hatua hiyo inalenga kuongeza matumizi ya bidhaa za ndani, kukuza ujuzi wa wazawa na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje.