DIRISHA LA USAJILI WA TUZO ZA SERENGETI 2026 KUFUNGULIWA KESHO

Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaa.

WIZARA ya Maliasili na Utalii imetangaza rasmi kufunguliwa kwa dirisha la usajili kwa wadau wa uhifadhi na utalii kuwania The Serengeti Awards 2026, huku ikiwasisitiza kutumia fursa hiyo kuonyesha kazi, ubunifu na mafanikio yao katika uhifadhi na uendelezaji wa utalii.

Dirisha la usajili litafunguliwa kesho Agosti 20, 2026 na kufungwa Septemba 30, 2026, kupitia tovuti rasmi ya tuzo hizo www.serengetiawards.go.tz, ambako wadau watapata taarifa kuhusu kategoria, vigezo na taratibu za kushiriki.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Dk. Thereza Mugobi, amesema Serengeti Awards zinafanyika kwa mara ya pili ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kutambua, kuthamini na kuenzi mchango wa wadau katika uhifadhi wa maliasili na urithi wa Taifa pamoja na uendelezaji wa utalii.

Amesema tuzo hizo zinalenga pia kutoa motisha kwa wadau kuboresha utendaji, kuhamasisha ubunifu na kuongeza ushindani wa Destination Tanzania.

Dk. Mugobi amesema mwaka huu kutakuwa na kategoria 63 katika makundi saba, ambayo ni People’s Choice Awards, Tourism Operator Awards, Tourism Guide Awards, Best Accommodation and Restaurant Services, Conservation Awards, Tourism Exhibitor Awards na Special Appreciation Awards.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Serengeti Awards, Hatibu Madudu, amesema idadi ya kategoria imeongezeka kutoka 56 mwaka jana hadi 63 mwaka huu, baada ya kupokea maoni kutoka kwa wadau na kufanya maboresho katika mchakato wa tuzo.

Madudu amesema baadhi ya maboresho yamezingatia changamoto zilizobainika katika mchakato wa mwaka uliopita, huku wananchi wakitarajiwa kushiriki katika mchakato wa kuwapata washindi wa baadhi ya kategoria.

Wadau kutoka ndani na nje ya Tanzania wanaruhusiwa kuwania tuzo hizo iwapo watatimiza vigezo vilivyowekwa. Serikali imewahakikishia wadau kuwa mchakato wa Serengeti Awards 2026 utasimamiwa kwa kuzingatia uwazi, usawa na uadilifu.