KURASINI KUHIFADHI MAKASHA 550,000, KUPUNGUZA FOLENI BANDARINI

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

SERIKALI inatarajia kupunguza msongamano wa makasha katika Bandari ya Dar es Salaam kupitia eneo jipya la Kurasini Logistic Park , litakalokuwa na uwezo wa kuhifadhi makasha 550,000 kwa wakati mmoja na kuhudumia makasha 700,000 kwa mwaka.

Eneo hilo linalomilikiwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) linatarajiwa kuwa miongoni mwa suluhisho la changamoto ya msongamano bandarini, kwa kuhamishia baadhi ya shughuli za ukaguzi na uhakiki wa makasha nje ya eneo la bandari.

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema katika eneo hilo kutakuwa na huduma za uhakiki wa nyaraka (verification), ukaguzi kwa mashine maalumu (scanning) pamoja na ukaguzi wa kimwili wa baadhi ya makasha.

“Huduma hizo zitaanza kwa makasha ya mizigo inayosafirishwa kwenda nje ya nchi (export), kabla ya kupanuliwa na kujumuisha makasha ya mizigo inayoingia nchini (import),”alisema Profesa Mbarawa.

Ameeleza kuwa mradi huo unatekelezwa na mwekezaji aliyepewa dhamana ya kuendesha Kituo cha Makasha Na. 2 (Terminal Two), ukiwa na lengo la kuongeza uwezo wa bandari na kuboresha ufanisi wa utoaji huduma.

Kutokana na umuhimu wa mradi huo, Mbarawa amezitaka Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha barabara maalumu zitakazounganisha eneo hilo zinakamilishwa kwa haraka.

Amesisitiza kuwa wasimamizi wa mradi, mkandarasi na wataalamu wanapaswa kuhakikisha kazi zilizobaki zinakamilika kwa wakati ili eneo hilo lianze kutumika kama ilivyopangwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam  Abeid Garus amesema kukamilika kwa eneo la Kurasini RORO Kipande kutapunguza msongamano wa magari na kuongeza uwezo wa bandari kupokea na kuhudumia shehena za makasha.

Aliema kuhamishia shughuli za scanning na verification katika eneo hilo kutapunguza shughuli zinazofanyika ndani ya bandari, hivyo kuongeza kasi ya upitishaji wa mizigo na kuboresha mtiririko wa magari.

Aliongeza kuwa eneo hilo litakuwa na mashine za kutosha za ukaguzi wa makasha, zitakazosaidia kuongeza ufanisi na kupunguza muda wa kuhudumia shehena.

Alisema kwa maandalizi yaliyofanyika, wanatarajia kuanza kulitumia eneo hilo Januari, likianza kama kituo cha muda (TD), kabla ya kuanza kutoa huduma kamili baada ya kuwasili kwa mashine za scanning.

Mradi huo unatajwa kuwa sehemu ya juhudi za kuboresha miundombinu na kuongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam katika kuhudumia biashara ya ndani na kimataifa.