PDPC YAANZA UKAGUZI MKALI WA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI NCHINI

Na Asha Mwakyonde, DODOMA

TAARIFA binafsi za wananchi zinazoendelea kukusanywa na kuchakatwa na taasisi, mashirika pamoja na wafanyabiashara nchini sasa zitawekwa chini ya uangalizi zaidi, baada ya Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC),kuanza ukaguzi wa uzingatiaji wa sheria katika maeneo mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 28, 2026 jijini Dodoma Mkurugenzi Mkuu wa PDPC, Dk. Emmanuel Mkilia, amesema ukaguzi huo unalenga kuhakikisha wakusanyaji na wachakataji wa taarifa binafsi wanazingatia matakwa ya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Sura ya 44.

Amesema katika ukaguzi huo, Tume itachunguza usajili wa taasisi katika rejesta ya Tume, utekelezaji wa majukumu ya Afisa Ulinzi wa Taarifa (DPO), pamoja na namna taarifa binafsi zinavyokusanywa, kuchakatwa na kuhifadhiwa.

Aidha,ameongeza kuwa PDPC itakagua utaratibu wa kusafirisha taarifa binafsi nje ya nchi kwa kuzingatia masharti ya Vifungu vya 31 na 32 vya Sheria hiyo.

Dk. Mkilia amesema Tume pia itachunguza hatua zinazochukuliwa na taasisi kulinda taarifa binafsi dhidi ya kupotea, kuharibiwa, kubadilishwa au kuchakatwa bila idhini, kwa mujibu wa Kifungu cha 27(1) cha Sheria.

Amesisitiza kuwa taasisi, mashirika na wafanyabiashara watakaobainika kukiuka matakwa ya sheria watachukuliwa hatua za kisheria, ikiwamo kupewa adhabu na faini kwa mujibu wa sheria.