RAIS DK.SAMIA KUWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA MATANGI YA MAFUTA KESHO

Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam

RAIS Dk.Samia Suluhu Hassan  anatarajia kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa matangi 15 yakuhifadhia mafuta yenye thamani ya Sh Bilioni 678.6 ambapo ni sehemu ya utanuzi wa bandari wenye lengo la kuongeza ufanisi.

Akizungumza leo Machi 2, 2026 jijini Dar es Salaam na  waandishi wa habari Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa alisema uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika katika eneo la  Kigamboni Mnadani jijini Dar es Salaam Februari 4 mwaka huu ambapo Dk. Samia  ataongoza tukio hilo ambalo ni muhimu kwa maendeleo ya sekta ya Uchukuzi na Uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Amesema  ujenzi wa matenki hayo unaonyesha dhamira ya kweli ya serikali ya awamu ya sita katika kuimarisha mikakati ya kupanua  miundombinu ya bandari nchini.

“Ujenzi wa matenki haya ni sehemu ya mkakati wakuongeza uwezo wa bandari unaoenda sambamba na  na ujenzi wa magati ambapo kwa sasa tumeanza na Gati namba moja ikiwa ni sehemu ya mkakati ya kuongeza uwezo wa bandari ya Dar es Salaam katika kuingiza shehena kubwa zaidi.

”Kila gati itakayojengwa itakuwa na urefu wa Kilomita 500 na uwezo wa kupokea meli mbili kwa wakati mmoja,kukamilika kwa mradi huu utakuwa na  uwezo wa kupokea tani Milion 60 kwa mwaka na kufanya bandari yetu kuwa miongoni mwa bandari zenye ushindani mkubwa,”amesema Profesa Mbarawa.

Profesa Mbarawa alisema katika kipindi cha Julai mpaka Disemba Mwaka jana,Bandari ya Dar es Salaam ilihudumia taribani Shehena za mizigo  tani Milioni 19.9 huku matarajio ya Serikali ni kufikia tani Milioni 40 mwisho wa mwaka 2025/26.

Amesema kiasi hicho cha ukuaji kimevuka malengo waliojiwekea jambo lilowalazimu kuendelea kupanua miundombinu ya bandari na kwendana na  mahitaji ya soko.”Serikali  inaendelea na ujenzi wa matenki 15 ya kuhifadhia mafuta yatakayoongeza uwezo wa kuhifadhi mafuta kwa mita za ujazo 378000 hatua  hii itapunguza muda kwa meli za mafuta kukaa bandarini na kutoka kwa wastani wa siku 3 badala ya siku 10.

”Hali hii itaweza kuongeza ufanisi kuvutia wawekezaji zaidi na kuimarisha usalama wa nishati hiyo,”amesema Profesa Mbarawa.

Aidha amesema maboresho hayo yanaenda na mkakati wa kuimarisha usafirishaji  wa mizigo kwa njia ya reli kupitia SGR katika  kuhakikisha kati ya asilimia 70 hadi 80 ya mizigo yote inaenda kwenye mtandao wa reli kusafirishwa.

Amesema kwa sasa zaidi ya asilimia 90 ya mzigo unaotoka bandari ya Dar es Salaam inapitia barabarani hiyo  maana yake ni kuwa barabara zinakufa,ajali zinakuwa nyingi,ucheleweshaji wa mizigo kutoka sehemu moja hadi nyingine na kusababisha  msongamano.

”Mizigo ikipita kwenye treni hali itakuwa nzuri zaidi,Sekta ya uchukuzi imeendelea kuwa muhimili muhimu  wa uchumi wa taifa kwa kuchangia zaidi  ya asilimia 40 ya mapato ya Serikali kupitia  kodi ya Forodha pamoja na kuingiza wastani wa Dola za Kimarekani Milioni 2.48 kwa mwaka kama fedha za kigeni kutoka wizara za uchukuzi za nchi za jirani,”amesema Profesa Mbarawa.