Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
MKUU wa Wilaya ya Ubungo, Mheshimiwa Albert Msando amefanya ziara ya kukagua hali ya maji katika Wilaya hiyo sambamba na kukagua utekelezaji wa mradi wa maji King’ong’o katika Kata ya Saranga ambao umeanza kutekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)utakaohudumia wakazi takribani 92,000 katika mitaa ya Michungwani, King’ong’o na Kimara B.
Mheshimiwa Msando ameipongeza DAWASA kwa juhudi wanazofanya katika kuboresha huduma ya maji kwa wananchi wa Ubungo akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha kazi inafanyika kwa viwango vya juu na kukamilika kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika haraka.

“Niipongeze DAWASA, lakini pia niishukuru Serikali kwa uwekezaji unaoendelea kufanyika katika Sekta ya maji. Nitoe rai kwa wananchi kujenga utamaduni wa kuhifadhi maji ili kuepuka ukosefu wa maji pindi changamoto za kihuduma zinapojitokeza,” amesema Mheshimiwa Msando.
Mwakilishi wa Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Modesta Mushi amebainisha kuwa utekelezaji wa mradi huo unafanyika kwa ubora na kwa kuzingatia weledi wa hali ya juu huku akihaidi kazi hiyo kukamilika mwanzoni mwa mwezi Novemba 2025.

Mheshimiwa Msando pia ametembelea mitaa ya Tarakea na Kavimbilwa eneo la Mbezi Makabe ambapo amejionea na kuridhishwa na hali ya upatikanaji wa maji katika eneo hilo.
