BASI LA KING MASAI TOWERS LAKAMATWA LIKISAFIRISHA SKANKA

Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imekamata kilogamu 9,689.833 za dawa za kulevya, pikipiki 11 na magari matatu likiwemo basi aina ya Scania la kampuni ya King Masai Tours, lenye namba za usajili wa nchi ya Msumbiji namba AAM 297 CA.

Basi hilo linalofanya safari zake za Dar es Salaam mpaka Msumbiji kupitia katika mikoa ya Kusini linadaiwa  kukarabatiwa maalum kwa shughuli hizo kwakuwa nusu la basi hilo limewekwa uwazi ambao umezibwa kwa ajili yakuficha dawa za kulevya ambapo limekamatwa likiwa na pakti 20 za skanka.

Akizungumza   jijini Dar es Salaam January 8, 2026 kuhusu basi hilo Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo amesema katika mtaa wa Wailes wilayani Temeke zilikamatwa pakiti 20 za skanka zenye uzito wa kilogramu 20.03.

Amesema dawa hizo zimekutwa ndani ya balo la mitumba na kufichwa kwenye basi hilo aina ya Scania la kampuni ya King Masai Tours, lenye namba za usajili wa chi ya Msumbiji namba AAM 297 CA.

“Basi hilo hufanya safari zake kati ya Nampula chini Msumbiji na Tanzania.Watuhumiwa waliokamatwa kuhusiana na tukio hilo ni Amasha Iddi Mrisho (40), mkazi wa Buza, Dar es Salaam na Seleman Juma Ally (32), raia wa Msumbiji,”amesema Kamishina Jenerali Lyimo.

Aidha amesema mmiliki wa basi hilo ni Mtanzania anayefahamika kwa jina la Martin Simon Kiando ambaye naye kwa sasa anaendelea kuhojiwa kwani kwa namna ambavyo basi hilo lilivyokarabatiwa yeye kama mmiliki atakuwa anajua.

Hata hivyo ametoa rai kwa wamiliki wa mabasi na vyombo vingine vya moto ambavyo vimefanyiwa marekebisho kwa lengo la kusafirisha dawa za kulevya waaache kwani mamlaka kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na salama wanafuatilia kwa karibu na sheria itachukua mkondo wake.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Aridhini (LATRA) Halima Lutavi amesema kutokana na tukio hilo LATRA wanamshikilia mmiliki wa basi hilo huku akieleza kuwa basi hilo halikuwa limesajiliwa nchini kwani aliomba usajili lakini alishindwa vigezo akaamua kusajili nchini Msumbuji.

 “Basi hilo halikusajiliwa kwasababu baada ya kampuni hiyo kuomba usajili alitakiwa kuleta basi likaguliwe kama linakidhi vigezo lakini pia ilitakiwa dereva wa basi naye awepo ili kuhakiki sifa kama anazo pamoja na kuingizwa katika mfumo kwa kupewa kitufe cha dereva.Hata hivyo baada ya kuwapa maelekezo hayo hajarudi tena.

“LATRA tumekuwa na utaratibu wa kukagua mabasi yote kwa kuangalia kadi inavyoelekeza kuhusu muundo wa bodi lakini katika nchi nyingine nazo zimekuwa na vigezo vya mabasi yake, hivyo tukio la kukamatwa kwa basi kwetu ni alamu na kwa kushirikiana na mamlaka nyingine tutafanya ukaguzi maalum.”