WAZIRI GWAJIMA AIPONGEZA TANESCO KUANDAA KONGAMANO LA WANAWAKE LA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dorothy Gwajima amelipongeza Shirika la umeme Tanzania TANESCO kwa kuandaa kongamano la wanawake wa Shirika hilo la kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ya umeme.

Mhe. Gwajima ametoa pongezi hizo jana Machi 04, 2026 wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo lililofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee akiwa kama mgeni rasmi ambapo amewataka wanawake wanaofanya kazi katika Shirika la Umeme Tanzania, (TANESCO), kuwa vinara wa mabadiliko katika kufanikisha ajenda ya taifa ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.

“Kongamano hili ni la kipekee sana na nimejionea namna tukio hili ni wazo zuri ambalo linalenga kutangaza na kukuza matumizi ya nishati ya kupikia hii ya umeme. Kongamano hili ni muhimu kwa sababu linagusa moja kwa moja afya zetu sisi wanawake ustawi wa familia zetu, maendeleo ya uchumi wa kaya na uhifadhi wa mazingira” Mhe. Doroth Gwajima – Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia wanawake na makundi maalumu

Waziri Gwajima alisisitiza kuwa wanawake wanayo nafasi ya kipekee ya kuhamasisha jamii kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na badala yake kutumia umeme kama nishati safi, salama na nafuu.

“Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazokabiliwa na changamoto ya nishati isiyosalama ya kupikia. Kwa mujibu wa sensa ya 2022 takriban asilimia 81.5 ya kaya nchini ilionesha hutumia nishati za kuni na mkaa kama Nishati kuu ya kupikia. Lazima tukitoka hapa baada ya kongamano hili tukaone namna nzuri nyingine ya kuboresha mikakati yetu twende tukahakikishe hii takwimu tunaipindua na wanarudi kwenye matumizi ya nishati ya kisasa ambayo ni salama na nafuu kwao” ameongeza Mhe. Gwajima

Aidha, aliwahimiza wanawake wa Shirika hilo kuwa mabalozi wa mabadiliko katika ngazi ya familia na jamii kwa kuondoa dhana potofu kuwa umeme ni ghali kwa matumizi ya kupikia na kueleza kuwa maendeleo ya teknolojia yameleta majiko yanayotumia umeme kidogo na yenye gharama nafuu, hivyo hakuna sababu ya kuendelea kung’ang’ania nishati zinazoharibu afya na mazingira.

Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO Balozi Zuhura Bundala amesema TANESCO imeendelea kuwa kinara katika kutoa elimu ya nishati safi ya kupikia.

“TANESCO imekuwa ikifanya vizuri kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia hususan nishati ya umeme ambayo ni nafuu na salama zaidi. Kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi nawapongeza sana wanawake wa Shirika hili kwa kuchagua ajenda hiyo muhimu” Balozi Zuhura Bundala – Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange, amesema nafasi ya wanawake ndani ya shirika hilo inaheshimika na kuthaminiwa katika ngazi zote za uongozi hivyo aliwataka kuwa makini na kuendelea kudumisha mshikamano.

“Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa wanawake wa TANESCO. Kwa wale ninaofanya nao kazi kwa ukaribu wamekua na mapenzi ya dhati kwangu. Wamenisaidia sana. Wamekuwa waaminifu na kwa kweli Mwenyezi Mungu atawalipa kwa kuwajibika” amesema Twange.

Aidha ameongeza kuwa uongozi wa TANESCO unatambua mchango wa wanawake katika safari ya kulifikisha Shirika mbele zaidi, akibainisha kuwa hakuna wakati ambao suala la kupandishwa vyeo au fursa mbalimbali limekuwa likipuuzwa bila kuzingatia usawa wa kijinsia.

Katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, Twange alieleza kuwa TANESCO linaungana na wanawake wengine duniani kuhimiza haki na usawa kwa wanawake na wasichana sambamba na utekelezaji wa maendeleo kupitia Dira ya Taifa 2050.

Kongamano hili ni moja ya mikakati ya TANESCO katika kutambua na kuthamini nguvu na jitihada za mwanamke ndani ya Shirika katika kuchagiza shughuli za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme nchini.