Na Mwandishi Wetu,Pwani
MAMLAKA ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupitia Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Matukio ya Sumu (NPCC), imewataka wananchi kuacha kutumia mawe kama njia ya kutibu madhara yanayotokana na kung’atwa na nyoka na badala yake kuwahi katika vituo vya afya ili kupata matibabu sahihi na kwa wakati.
Wito huo ulitolewa na Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Matukio ya Sumu, Yohana Goshashy, amesema hayo leo wakati akitoa elimu kwa wananchi wa Kibaha mkoani Pwani, kuhusu namna ya kujikinga na matukio ya kung’atwa na nyoka, hatua zinazopaswa kuchukuliwa endapo mtu atang’atwa na nyoka pamoja na madhara yanayoweza kujitokeza iwapo mhanga hatapata huduma ya kitabibu kwa wakati.

Goshashy alisema kuwa bado kuna baadhi ya wananchi wanaamini matumizi ya mawe kama tiba ya kuondoa sumu baada ya kung’atwa na nyoka, jambo ambalo amewataka wananchi kuliacha na badala yake kuhakikisha mgonjwa anapelekwa haraka katika kituo cha afya au hospitali.
“Tunawasihi wananchi kuacha kutumia mawe kama dawa ya kutibu mtu aliyeng’atwa na nyoka. Mtu anapong’atwa na nyoka anapaswa kuchukuliwa kama mgonjwa anayehitaji huduma ya kitabibu na apelekwe hospitali haraka iwezekanavyo. Tusipoteze muda katika tiba ambazo hazijathibitishwa kitaalamu,” alisema Goshashy.
Aliongeza kuwa, hatua ya kuwahi hospitalini ni muhimu kwa kuwa wataalamu wa afya wanaweza kufanya tathmini ya hali ya mgonjwa na kutoa huduma kulingana na madhara yaliyotokana na kung’atwa na nyoka.

Aidha, amewataka wananchi kutotumia njia za kienyeji ambazo zinaweza kuongeza madhara kwa mgonjwa, ikiwemo kuchanja sehemu iliyong’atwa, kunyonya damu au sumu, kuchoma eneo lililong’atwa au kufunga kiungo kwa nguvu bila ushauri wa kitaalamu.
Goshashy amesema wananchi wanapaswa kuwa na uelewa kwamba matukio ya kung’atwa na nyoka yanaweza kutokea katika maeneo mbalimbali, hususan katika maeneo ambayo shughuli za wananchi zinahusisha kilimo, ufugaji, uwindaji au shughuli nyingine zinazowaweka katika mazingira ambayo wanaweza kukutana na nyoka.
Kwa upande wao wananchi walioshiriki katika mafunzo hayo, wameeleza kuwa matukio ya kung’atwa na nyoka yamekuwa changamoto katika baadhi ya maeneo, huku wakisema wakati mwingine waathirika hukumbana na changamoto ya kufika hospitalini kwa wakati kutokana na umbali wa vituo vya afya. Na pia changamoto nyingine ni hofu na ukosefu wa uelewa wa kutosha kuhusu hatua sahihi za kuchukua mara baada ya mtu kung’atwa na nyoka.


