Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAVULANA wameongoza wasichana katika matokeo ya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) mwaka 2026, wakipata ufaulu wa asilimia 86.18 dhidi ya asilimia 84.43 za wasichana.
Hata hivyo, ufaulu wa jumla umeongezeka hadi asilimia 85.22 mwaka huu kutoka asilimia 81.80 mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 3.42.
Akizungumza leo Novemba 3, 2026 jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Profesa Said Mohamed, alisema ufaulu wa wavulana umeongezeka kwa asilimia 3.67 kutoka asilimia 82.51 mwaka jana, huku wasichana ukiongezeka kwa asilimia 3.22 kutoka asilimia 81.21.
Alisema jumla ya watahiniwa 1,168,718 walisajiliwa kufanya mtihani huo, wakiwemo wasichana 637,214 sawa na asilimia 54.52 na wavulana 531,504 sawa na asilimia 45.48.
Hata hivyo, kati ya waliosajiliwa, watahiniwa 1,139,318 sawa na asilimia 97.48 walifanya mtihani, huku 29,400 sawa na asilimia 2.52 wakishindwa kufanya.

Katika matokeo hayo, watahiniwa 970,876 wamefaulu kwa kupata madaraja ya A, B na C, huku 429,667 sawa na asilimia 37.72 wakipata madaraja ya juu ya A na B.
Kwa upande wa masomo, Kiswahili limeongoza kwa ufaulu wa asilimia 93.13, likifuatiwa na Uraia na Maadili kwa asilimia 90.12.
Masomo mengine ni Sayansi na Teknolojia (asilimia 80.34), Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi (asilimia 76.53), Hisabati (asilimia 62.56) na Kiingereza (asilimia 50.50).
Hata hivyo, Sayansi na Teknolojia limeonesha kushuka kwa ufaulu kwa asilimia 4.09 kutoka asilimia 84.43 mwaka jana hadi asilimia 80.34 mwaka huu.

Aidha, ubora wa ufaulu katika somo hilo kwa watahiniwa waliopata madaraja ya A na B umeshuka kutoka asilimia 48.14 mwaka jana hadi asilimia 33.60 mwaka huu.
Katika hatua nyingine, Profesa Mohamed alisema NECTA imezuia kutoa matokeo ya watahiniwa 371 waliougua na kushindwa kufanya mtihani katika masomo mengi au yote, huku wakipewa nafasi ya kurudia mtihani mwaka 2027.
Alisema pia matokeo ya watahiniwa 26 yamefutwa kutokana na udanganyifu, huku wengine watano wakifutiwa matokeo baada ya kubainika kuandika lugha ya matusi kwenye karatasi zao za majibu.

Kuhusu upatikanaji wa matokeo, alisema mwaka huu majina ya watahiniwa hayataoneshwa kutokana na kuzingatia Sheria na Kanuni za Ulinzi wa Taarifa Binafsi, badala yake namba za mtihani zitatumika kuwatambua.
Alisema matokeo hayo yatawasilishwa katika mamlaka husika kwa ajili ya kufanya uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga na elimu ya sekondari.


