Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
VIONGOZI wa dini katika madhebu mbalimbali nchini wameshauriwa kuacha kufanya siasa na wala kuwa sehemu ya kuwa wachochezi kwakuwa wao ni sehemu ya kimbilio pale ambapo nchi itakuwa na changamoto huku wakikumbushwa wajibu wa kuliombea Taifa la Tanzania hasa katika mwaka huu wa Uchaguzi Mkuu.
Pia kwa waumini wa dini mbalimbali ambao ni wanasiasa wamekumbushwa na kuhimizwa kufanya kampeni za kistaarabu lakini wawe wenye kujishusha na kusamehe kwani kila mmoja wetu analojukumu la kuhakikisha amani,umoja na mshikamano unaendelea kuwepo.

Hayo yameelezwa na Wachungaji kutoka Tanzania na Kenya wa Kanisa la Wadventista Wasabato walipokuwa wakihitimisha Wiki ya Uamsho iliyokuwa na maombi mbalimbali yakiwemo ya kuliombea amani ,umoja na mshikamano Taifa la Tanzania ambalo Oktoba mwaka huu linatatajia kufanya uchaguzi Mkuu .
Wiki ya Uamsho imeandaliwa na Kwaya ya Gethsemane Group Kinondoni (GGK) kutokea Kanisa la Wadventista Wasabato Kinondoni Jijini Dar es Salaam ambapo katika maombi hayo pia wamewaalika wachungaji wa Kanisa hilo kutoka nchini Kenya.
Akizungumza baada ya kufanyika kwa maombi ya kuliombea Taifa, Katibu wa Jimbo la Mashariki Kati mwa Tanzania wa Kanisa la Waadvestita Wasabato Tanzania Mchungaji Shashi Musa Wanna amesema walikuwa na maombi katika juma zima ambapo wametumia nafasi hiyo kuwa na mahubiri pamoja na maombi.
“Tulikuwa na wiki ya Uamsho wa kiroho katika Kanisa letu lakini pia kuliombea Taifa letu na Wachungaji wenzetu kutoka Kenya ambao tulikuwa nao wenzetu wanauzoefu mkubwa mambo ya siasa yanayoendelea Kenya.Tumehimiza maombi na umuhimu wa amani katika nchi yetu.
“Kwasababu bila amani nchi haiwezi kutawalika lakini sisi kama Wakristo bila amani hatuwezi kufanya kazi ya Injili,hatuwezi kupata uhuru wa kuabudu .Tumeshirikiana kuliombea Taifa letu nasi kama Watanzania tunawashukuru wachungaji wenzetu maana wamekuja kutuamsha kutuonyesha umuhimu wa maombi na kumtegemea Mungu
“Kanisa la Wadventista Wasabato tunatoa rai kwa waumini wetu tuendelee kuliombea Taifa hasa mwaka huu wa uchaguzi na kama Kanisa hatuingii kwenye siasa lakini tunawaumini wetu ambao wanaweza kuwa wanasiasa wakafanya siasa .Wafanye siasa za kistaarabu,”amesema Mchungaji Wanna.
Aidha amesema pia wanawashauri viongozi wengine wa dini wasiwe wanasiasa kwani viongozi wa dini ni sehemu ya kimbilio pale ambapo nchi itakuwa na shida hivyo wanawajibu wa kuombea Taifa lakini wanakazi ya kufanya usuluhishi kwa maana ya waumini wao pia ni sehemu ya wanasiasa.
Pia amesema wanawaambia waumini wawe ni wenye kusamehe na kujishusha huku akiendelea kutoa rai kwa viongozi wengine wa dini nchini kuliombea Taifa letu.”Tusiwe sehemu ya uchochezi bali tuwe sehemu ya kuleta amani kwa maombi na ushauri.”
Kwa upande wake Mhubiri kutoka nchini Kenya Mchungaji Patrick Muthee amesema katika zama hizi ambazo Dunia imeharibika wakati mwingine makanisa na waumini wake wanajaribiwa huku akieleza Kanisa linapoongia katika siasa kunakuwa na changamoto kwasababu ile roho ya Mungu inaondoka
“Kazi ya Kanisa ni kuleta watu pamoja na tunatambua viongozi Mungu ndio huchagua sisi kama waumini Mungu anatutumia katika hali ile ya kupiga kura lakini Mungu anajua njia iliyobora.Hivyo kama Kanisa viongozi,wachungaji , na masheikh tuzungumze na waumini wetu ….
“Kuwaambia jukumu kubwa la kuchagua viongozi ni la Mungu hivyo tumtangulize Mungu, wawe na imani Mungu ndiye anatuchagulia viongozi hatutakuwa na mashindano ,hatutakuwa na vurugu.
“Tunawaomba watulie na siku ya kupiga kura wajue kila mmoja ni ndugu wa mwinzie wale walioupinzani,wale walioserikalini wote ni wamoja na atakayechaguliwa awe wa upinzani au chama tawala yeye ni mmoja wa wale waumini na raia wa nchi moja,”amesema Mchungaji Muthee
Wakati huo huo Mchungaji Haruni Muturi wa Kanisa la Wadventista Wasabato kutoka nchini Kenya amesema katika wiki hiyo ya uamsho wametumia nafasi hiyo kujihoji miyoni mwao na kujitoa upya kwa Yesu Kristo kwasababu wanajua kuna majaribu.
“Na kwasababu ya majaribu hayo Mungu aweze kusikia watu wake ,kuwarejesha katika upendo wake na jinsi tulivyokuwa tumekuja kuombea nchi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hilo nalo ni jambo tumelizingatia sana.
“Kwasababu tunataka waumini wasiwe na vita na Serikali ,wafahamu jinsi ya kufanya kampeni za kuchagua viongozi kwa ustaarabu na wawe watii na kuweka Serikali katika Maombi badala ya vita ,ni jukumu letu pia kuendelea kuomba mpaka uchaguzi utakapokwisha Oktoba mwaka huu.
“Wachungaji wote ni mabalozi wa nchi ya mbinguni hivyo tunapaswa kufanya maombi mara nyingi na kwasababu tunajua kwamba vurugu ambazo ziko katika nchi nyingine zinaweza kuondolewa kupitia maombi.Pengine tumelala katika kazi yetu ya kufanya maombi na ndio maana unasikia kuna nchi zipo katika machafuko.”
Awali Mchungaji wa Kanisa la Waadvestita Wasabato Kinondoni Victor Geofrey amesema wamekuwa katika wiki ya Uamsho iliyokuwa na lengo la kukumbushana mambo muhimu katika maisha ya Kikristo na kusimama kama Kristo alivyofundisha na hasa wakijua wako siku za mwisho naye anakaribia kuja upesi .
“Lakini katika wiki ya Uamusho pia tumeomba kwa mambo mbalimbali kwa ajili ya maisha ya kiroho lakini pia kwa ajili ya mambo ya taifa letu la Tanzania kwani tuko katika wakati uliomakini ambao kila Mtanzania anatakiwa kuchukua jambo hilo kwa umakini wake.
“Tumeliombea Taifa amani na mshikamano na tumehitimisha siku ya ya Sabato, siku ya ibada kwa pamoja na tumekutana kumshukuru kwa kuwa ametusikia kwa wiki nzima na maombi haya yatakuwa endelevu kwasababu tumeamshwa maombi ni maisha ya kila siku ya wale ambao wanatazamia maisha ya kiroho.
“Tutaendelea na maombi ya kiroho na taifa letu kwasababu ndiko mahali tunaishi tunatamani ya kwamba watu wamjue Mungu zaidi pale panapokuwa na amani na utulivu ndivyo maandiko yanavyotuambia.”