WATAHINIWA 134,390 KUFANYA MTIHANI KIDATO CHA SITA LEO

Na Aziza Masoud,Dar es Salaam

JUMLA ya watahiniwa 134,390 wamesajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha sita (ACSEE) mwaka 2025  unaotarajiwa kuanza leo Mei 5 hadi 26 mwaka 2025.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) Dk.Said Mohamed alisema  kuanza kufanyika Kwa mitihani hiyo ya kidato kutaenda sambamba na mitihani  ya ualimu katika ngazi ya cheti na stashahada  ambao utamalizika Mei 19 ambapo watahiniwa 10,895 wamesajiliwa kufanya mitihani huo.

Alisema ambapo kati ya watahiniwa 134,390  waliosajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha sita 126,957 ni wa shule huku watahiwa 7,433 wakujitegemea.

“Kati ya watahiniwa wa shule 126,957 waliosajiliwa wavulana ni 64,581 sawa na asilimia 50.87 na wasichana ni 62,376 sawa na asilimia 49.13,”alisema Dk.Mohamed.

Alisema katika idadi hiyo ya watahiniwa pia wamo wenye mahitaji maalum ambao ni 453 ambapo kati yao wenye uoni hafifu ni 300,wasioona ni 16,wenye uziwi 58,wenye ulemavu wa akili ni wanne huku watahiniwa 75 wana ulemavu wa viungo vya mwili.

Alisema kati ya watahiniwa wakujitegemea 7,433 waliosajiliwa wavulana ni 4,782 sawa na asilimia 64.33 na wasichana ni 2,651 sawa na asilimia 35.67.

“Katika idadi hiyo ya watahiniwa wakujitegemea pwamo watahiniwa wenye mahitaji maalum 151 ambapo kati ya hao wenye uoni hafifu 142 na wasioona ni tisa,”alisema Dk.Mohamed.

Alisema idadi hiyo ya watahiniwa wakujitegemea ikilinganishwa na mwaka 2024 ina ongezeko la watahiniwa 20,854 sawa na asilimia 18.37 kwa mwaka 2025 ikilinganishwa na mwaka 2024 ambapo watahiniwa waliosajiliwa walikuwa 113,536.

Akizungumzia kuhusu mtihani wa ualimu Dk.Mohamed jumla ya watahiniwa 10,895 wamesajiliwa kufanya mtihani wa ualimu  ambapo kati ya watahiniwa hao 3,100 ni wa ngazi ya stashahada na 7,795 ni wa ngazi ya cheti.

“Kwa ngazi ya stashahada wanaume ni 1,349 sawa na asilimia 56.48 na wanawake ni 1,349 sawa na asilimia  43.52.

“Aidha kwa ngazi ya cheti watahiniwa 3,987 sawa na asilimia 48.85 ni wanaume na watahiniwa 3,808 sawa na asilimia 51.15 ni wanawake,”alisema Dk.Mohamed.

Alisema watahiniwa wenye mahitaji maalum waliosajiliwa kufanya mtihani wa ualimu ni 23 kati ya hao wawili wana uoni hafifu,watatu wasioona,mmoja kiziwi na mmoja mwenye ulemavu wa viungo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *