JAB KUTOA ITHIBATI YA MAISHA KWA WAANDISHI WAKONGWE

Na Aziza Masoud, Dar es Salaam

BODI  ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imezindua  rasmi Mwongozo wa Ithibati ya Maisha  unaoruhusu waandishi wakongwe ambao hawana vigezo vya elimu vilivyowekwa kupata ithibati maalum kwakuzingatia uzoefu walionao katika taaluma ya habari.

Uzinduzi wa muongozo huo umefanyika katika  siku maalum ya JAB yaani ‘JAB Day’ ndani ya kijiji cha Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo katika  viwanja vya Maonesho  ya 50  ya  Biashara ya Kimataifa Sabasaba.

 Kwa mujibu wa muongozo huo watakaopata Ithibati ya Maisha ni  waandishi waliokuwa na umri wa miaka 50 au zaidi wakati Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 ilipoanza kutumika na ambao walikuwa tayari wametoa mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya habari.

Akisoma taarifa ya  Mwenyekiti wa JAB, Tido Mhando, iliyosomwa na mjumbe wa Bodi hiyo  Dkt. Egbert Mkoko, ilieleza kuwa mwongozo huo unawahusu wandishi wa kada hiyo kwa sababu hawakupata nafasi ya kufikia kiwango cha diploma kutokana na mazingira ya wakati husika, lakini walijifunza kwa vitendo na kujenga uzoefu uliowafanya kuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya vyombo vya habari na ujenzi wa taifa.

Taarifa ya Tido imeeleza kuwa hatua hiyo inalenga kuhifadhi historia ya taaluma ya uandishi wa habari, kuthamini mchango wa waandishi wa kizazi cha mwanzo na kuhakikisha maarifa pamoja na uzoefu wao vinaendelea kuwa sehemu ya urithi wa tasnia hiyo.

Bodi hiyo pia imepongeza ushirikiano unaoendelea kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo katika kuimarisha taaluma ya uandishi wa habari, huku ikisisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili, weledi na uwajibikaji kwa wanahabari.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa JAB, Patrick Kipangula, alisema uzinduzi wa Mwongozo wa Ithibati ya Maisha unaonesha dhamira ya bodi ya kuhakikisha inathamini mchango wa waandishi wakongwe pamoja na kusimamia viwango vya taaluma kupitia sheria.

“Sisi kama JAB tutaendelea kuutambua  mchango wa waandishi wa habari wakongwe,kuuheshimu  na utakuwa kuwa sehemu ya historia ya maendeleo ya sekta ya habari nchini,”alisema Kipangula.