Na Mwandishi Wetu Dar es Salaam
SHIRIKA ya Mawasiliano Tanzania (TTCL) imesema kupitia shughuli zake mbalimbali zikiwemo intaneti liimeendelea kutoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa kidijitali nchini.
Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Meneja wa Mahusiano wa TTCL,Ester Mbanguka alisema shirika ambalo ni namna moja katika kasi ya intaneti nchini kutokana na uwekezaji wake katoka mkongo wa Taifa limekuwa likitoa huduma zake za intaneti zenye kasi kubwa zinazowawezesha wananchi kupata huduma hiyo kwa haraka.

Alisema kupitia huduma ya intaneti wananchi, wafanyabiashara na watengenezaji wa maudhui kutumia teknolojia kwa ufanisi zaidi katika shughuli zao za kila siku ambapo wengi wao zinawaingizia kipato.
Alisema TTCL wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha Watanzania wanapata huduma za mawasiliano zenye ubora wa hali ya juu zinazorahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii.

“Kupitia huduma zetu za intaneti zenye kasi kubwa, tumekuwa tukichangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa kidijitali. Watu wengi hasa wasanii na watengeneza maudhui wanafanya biashara mtandaoni, wanatoa huduma kwa wateja wao kwa haraka na kwa ufanisi zaidi,” alisema.
Alisema watengenezaji wa maudhui mtandaoni wameendelea kunufaika na huduma ya Super Experience ya TTCL inayowawezesha kufanya kazi zao bila kukumbwa na changamoto za kukatika kwa mtandao.

“Watengenezaji wa maudhui wanahitaji intaneti yenye kasi na uthabiti mkubwa. Kupitia huduma yetu ya Super Experience, wanaweza kupakia maudhui, kufanya matangazo ya moja kwa moja na kuendesha biashara zao za kidijitali kwa ufanisi mkubwa,” alisema.
Aliongeza kuwa mbali na biashara za mtandaoni,huduma za TTCL zimeendelea kutumiwa katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, burudani na michezo ya mtandaoni (online games), ambapo watumiaji wanafurahia huduma yenye kasi na uthabiti mkubwa.

Mbanguka aliwataka Watanzania kutembelea banda la TTCL lililopo katika maonesho ya Sabasaba ili kujionea huduma na bidhaa mbalimbali zinazotolewa na kampuni hiyo.
“Katika banda letu tunatoa huduma mbalimbali ikiwemo usajili wa laini bure, mauzo ya router na modem, pamoja na suluhisho za mawasiliano kwa wafanyabiashara na watu binafsi. Pia tumewawezesha wageni kutumia huduma ya Free Wi-Fi ili wajionee ubora wa mtandao wetu,” alisema.

Alisema Sabasaba ya mwaka huu imekuwa fursa muhimu kwa wananchi kupata elimu kuhusu huduma za kisasa za mawasiliano pamoja na suluhisho mbalimbali vinavyotolewa na TTCL.
Alisisitiza ,huduma inayovutia zaidi wateja wanaotembelea banda la TTCL ni intaneti ya Fiber Mlangoni Kwako inayotolewa kwa makazi na ofisi.


