Na Aziza Masoud, Dar es Salaam
KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO), CPA Jeremiah Mgeta, amesema taasisi hiyo imejipanga kuhakikisha vyama vyote vya ushirika nchini vinakaguliwa katika mwaka wa fedha 2026/27 ili kuimarisha uwajibikaji, uwazi na kuongeza imani ya wanachama.
CPA Mgeta alitoa kauli hiyo alipotembelea banda la Wizara ya Kilimo katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo alisema ushirika una mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya kilimo na uchumi wa taifa kupitia usimamizi mzuri wa rasilimali za wanachama.
“Ukaguzi unaofanywa na COASCO ni nguzo muhimu ya kujenga uwazi, uwajibikaji na kuimarisha imani ya wanachama katika vyama vya ushirika, hali inayochochea ukuaji wa sekta hiyo na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya uchumi wa nchi,”alisema CPA Mgeta.

CPA Mgeta amesema ukaguzi huo utalenga kuwapa wanachama taarifa sahihi kuhusu hali ya vyama vyao pamoja na kuhakikisha vinafuata sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji.
Alisema COASCO, kama jicho la Serikali katika usimamizi wa vyama vya ushirika, huandaa ripoti ya kila mwaka inayoonyesha matokeo ya ukaguzi na kutoa maoni kuhusu mwenendo wa vyama hivyo.
“Katika mwezi Septemba mwaka huu tutatoa ripoti maalumu ya matokeo ya ukaguzi wa mwaka 2025/26 kwa wananchi, wanahabari na wadau wa ushirika ili wajue hali halisi ya usimamizi wa vyama vya ushirika nchini,” alisema.
Aidha, amesema awamu ya kwanza ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha 2026/27 itaanza rasmi Julai 20, huku akivitaka vyama vya ushirika kuandaa na kuwasilisha taarifa zao za fedha za mwaka 2025/26 katika ofisi za COASCO zilizopo karibu katika mikoa yote ya Tanzania Bara.
Alisisitiza umuhimu wa vyama kuandaa taarifa za fedha kwa kuzingatia sheria na viwango vinavyotakiwa ili kupunguza hoja zinazojitokeza wakati wa ukaguzi.

CPA Mgeta amesema hatua zinazochukuliwa na Serikali pamoja na maboresho ya usimamizi zimeanza kuzaa matunda, akieleza kuwa idadi ya vyama vinavyopata hati safi za ukaguzi imeongezeka kutoka asilimia 4 miaka ya nyuma hadi kufikia asilimia 16 kwa sasa.
Pia alisema idadi ya hati zenye maoni imeendelea kupungua ikilinganishwa na miaka iliyopita, jambo linaloashiria kuimarika kwa usimamizi wa fedha na utawala ndani ya vyama vya ushirika.
Amebainisha kuwa mbali na ukaguzi, COASCO inaendelea kutoa huduma za ushauri kwa vyama vya ushirika kuhusu uandaaji wa taarifa za fedha, uzingatiaji wa sheria za kodi, utawala bora na mifumo ya uendeshaji ili kuviwezesha kufanya kazi kwa ufanisi.


