Na Aziza Masoud,Dar es Salaam
MAMLAKA ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imewahimiza wananchi kutembelea banda lake katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) ili kupata elimu kuhusu huduma za maabara, matumizi salama ya kemikali na uchunguzi wa sampuli mbalimbali.
Akizungumza katika maonesho hayo, Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Bidhaa na Mazingira wa GCLA, Dk. Shimo Peter Shimo, amesema mamlaka hiyo ndiyo maabara ya rufaa nchini inayofanya uchunguzi wa sampuli mbalimbali, zikiwemo zinazohusiana na makosa ya jinai, ubora na usalama wa bidhaa pamoja na uchafuzi wa mazingira kwa lengo la kulinda afya za wananchi na mazingira.

Amesema GCLA imepanua huduma zake katika kanda mbalimbali nchini ili kuwafikishia wananchi huduma kwa ukaribu zaidi. Kanda hizo ni pamoja na Nyanda za Juu Kusini (Mbeya), Kaskazini (Arusha), Kati (Dodoma), Kusini (Mtwara na Songea), Ziwa (Mwanza na Geita) pamoja na Kanda ya Mashariki (Tanga).
Dk. Shimo amesema mamlaka hiyo pia inasimamia matumizi salama ya kemikali za viwandani na majumbani kwa mujibu wa Sheria Na. 3 ya mwaka 2003, pamoja na kusimamia sheria zinazohusu vinasaba vya binadamu na kuhakikisha maabara zote zinazofanya uchunguzi wa kemikali nchini zinazingatia viwango vinavyotakiwa.

Ameeleza kuwa GCLA imepewa mamlaka ya kusimamia maabara zote za kemikali nchini ili kuhakikisha zinatoa matokeo yenye ubora na yanayokubalika kitaifa na kimataifa.
Katika Maonesho ya Sabasaba, Dk. Shimo amesema wataalamu wa GCLA wanatoa elimu kuhusu namna ya kuwasilisha sampuli kwa uchunguzi, matumizi salama ya kemikali, taratibu za usajili kwa wanaojihusisha na kemikali pamoja na huduma nyingine zinazotolewa na mamlaka hiyo.

Aidha, amesema maabara zote za GCLA zimepata ithibati ya kimataifa, jambo linalowapa wananchi na wadau uhakika kuwa matokeo ya uchunguzi yanayotolewa yanatambulika na kukubalika katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.
Amewataka wananchi kutumia fursa ya maonesho hayo kutembelea banda la GCLA ili kupata elimu na huduma mbalimbali zinazolenga kulinda afya, usalama wa bidhaa na mazingira.


