Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) wamezindua Nyumba Janja yenye mfumo wa kisasa wa unaosaidia kuongeza usalama wa nyumba kwa kupunguza hatari za majanga kama moto na ajali nyingine zinazosababishwa na hitilafu za umeme pindi zinapojitokeza.
Nyumba hiyo janja ambayo ni kivutio kikubwa katika Maonesho Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es salaam (DITF) maarufu kama Sabasaba kwakuwa ina teknolojia inayorahisha matumizi ya umeme kwa kumwezesha mtumiaji kudhibiti vifaa vya umeme kwakutumia programu maalum akiwa popote.

Akizungumza katika banda la TANESCO lililopo Sabasaba,Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa wateja wa TANESCO, Irene Gowele teknolojia hiyo italenga kuongeza ufanisi wa maumizi ya umeme na kuboresha maisha ya watanzania na itawawezesha wananchi kuelewa kwa vitendo thamani ya matumizi ya umeme katika maisha ya kila siku.
Alisema teknolojia hiyo inamwezesha mtumiaji kudhibiti vifaa vya umeme kwa kutumia programu maalumu (application) kwenye simu ya mkononi. kupitia mfumo huo ambapo mteja anaweza kuwasha au kuzima vifaa vya umeme akiwa mahali popote duniani, sambamba na kufuatilia kiwango cha matumizi ya umeme wa kila kifaa ili kupunguza gharama za matumizi.

“Teknolojia hii inawasaidia wateja kudhibiti matumizi ya umeme kwa ufanisi zaidi. Pia ndani ya nyumba hiyo tumeweka vifaa vinavyotumia umeme kwa ufanisi (energy efficient appliances), ambavyo vinatumia umeme kidogo lakini vinatoa huduma bora,” amesema Gowele.
Mbali na Nyumba Janja, TANESCO inaendelea kutekeleza mpango wa kuwawezesha wananchi kutumia nishati safi yakupikia kwakuuza majiko ya umeme kwa njia ya mkopo.

Gowele amesema wananchi wanaotembelea banda la TANESCO wanaweza kununua au kukopa majiko hayo kwa kuwasilisha namba ya mita ya umeme pamoja na Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIDA) kwa ajili ya kuthibitisha taarifa zao kama wateja wa TANESCO.
Ameeleza kuwa majiko hayo n yanatumia umeme mdogo na yana uwezo wa kupika vyakula mbalimbali vya Kitanzania kwa gharama ya ndogo.

Katika maonesho hayo, TANESCO pia inatoa fursa kwa wananchi kujionea kwa njia ya teknolojia ya kidijitali baadhi ya miradi mikubwa ya uzalishaji umeme nchini, ikiwemo Kituo cha Kufua Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP) pamoja na mradi wa kwanza mkubwa wa kuzalisha umeme kwa nishati ya jua uliopo Kishapu mkoani Shinyanga wenye uwezo wa kuzalisha megawati 50.
Vilevile, shirika hilo linaendelea kuelimisha wananchi kuhusu matumizi ya vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme kama gari na bajaji za umeme.


