TPDC YAPANUA MATUMIZI YA GESI ASILIA MAJUMBANI

Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam

SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)  amesema  imejipanga kuongeza idadi ya nyumba  zitakazounganishwa  na huduma ya gesi asilia  kwa ajili ya kupikia majumbani ambapo wanatarajia kuunganisha nyumba zaidi ya 1000.

Akizungumza katika Maonesho ya Biashara ya 50 yanayofanyika  katika Viwanja vya Maonesho ya Biashara ya Dar es Salaam (DTIF) ,Afisa Masoko wa TPDC, Neema Cleophace nyumba hizo zipo katika mkakati wa kuongeza idadi ya watumiaji wa gesi ya kupikia majumbani ambapo mpaka sasa zaidi  nyumba 2,500 zimeshaunganishwa na matumizi ya geso asilia.

“TPDC tumejipanga kuongeza idadi ya nyumba zitakazounganishwa na huduma ya gesi asilia kwa ajili ya kupikia,kwa Dar es Salaam tunatarajia kuunganisha zaidi ya nyumba 1,000,pia tuna mpango wa kuunganisha zaidi ya nyumba 800 katika Wilaya ya Mkuranga na zaidi ya nyumba 800 katika mkoa wa Mtwara,” alisema.

Alisema linaendelea na jitihada za kuongeza matumizi ya gesi asilia nchini, hususan katika sekta ya kupikia, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwawezesha kutumia nishati safi na salama.

Akizungumzia kuhusu matumizi ya gesi ya asilia alisema takribani asilimia 70 ya gesi asilia inayozalishwa nchini hutumika kuzalisha umeme.

Alisema matumizi ya gesi asilia kwenye sekta ya usafiri nayo yanaendelea kukua ambapo zaidi ya magari 5,000 tayari yanatumia nishati hiyo, yakihudumiwa na vituo zaidi ya 18 vya kujazia gesi asilia vilivyopo nchini.

Aidha, alisema zaidi ya viwanda 59 nchini vinatumia gesi asilia katika shughuli zao za uzalishaji kutokana na faida zake za kupunguza gharama za nishati na salama.

Alitoa wito kwa wananchi kutembelea banda la TPDC katika Maonesho ya Sabasaba ili kujifunza kuhusu shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na shirika hilo, pamoja na kupata elimu kuhusu matumizi na faida za gesi asilia katika maisha ya kila siku.