WAZIRI HOMERA: SHERIA IMARA NI NGUZO YA MAENDELEO YA UCHUMI

Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM

WAZIRI HOMERA: SHERIA IMARA NI NGUZO YA MAENDELEO YA UCHUMI

Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Katiba na Sheria,Dk. Juma Homera, ameeleza kuwa
marekebisho ya sheria zinazohusu uingizaji wa bidhaa nchini yameendelea kuboresha mazingira ya biashara na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Dk. Homera ameyasema hayo Julai 3, 2026 alipotembelea banda la Wizara hiyo katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF),maarufu ‘Sabasaba’
ambapo amesema kuwepo kwa maika 50, ya maonesho hayo kumekuwapo na mafanikio makubwa, yakiwemo marekebisho ya sheria mbalimbali ambayo yamechangia kukuza uchumi, kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuwanufaisha wananchi.

Aidha amewahimiza wananchi kuzingatia na kutekeleza sheria za nchi, akisisitiza kuwa kuvunja sheria kutasababisha wahusika kuchukuliwa hatua na vyombo vinavyosimamia utekelezaji wa sheria.

Waziri huyo ameeleza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeweka mkazo katika kulinda haki za binadamu, kuimarisha utawala bora, uwazi na uwajibikaji, misingi ambayo ni muhimu katika kuleta maendeleo endelevu.

Dk.Homera amesema wizara hiyo imejipanga kuendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, huku ikilenga kufanya vizuri zaidi kuliko ilivyofanya mwaka uliopita.

“Wananchi wanaofuatilia utendaji wa taasisi za Umma wanafahamu ni nani anayetoa huduma bora. Mwaka uliopita tulifanya vizuri sana, lakini huu ni mwaka mwingine na tuna nafasi ya kufanya vizuri zaidi,” amesema.

Amesema kwa sasa huduma mbalimbali zimeboreshwa, ikiwemo utoaji wa nyaraka muhimu kama vyeti vya kuzaliwa, ndoa na vifo, ambazo zinaweza kupatikana ndani ya saa 48.

Dk. Homera amewataka wananchi kufika katika banda la Wizara ya Katiba na Sheria ili kupata huduma mbalimbali za msaada wa kisheria, akieleza kuwa wizara hiyo imeweka mazingira yatakayowawezesha kupata ushauri wa kisheria pamoja na kuunganishwa na mawakili watakaowasaidia kushughulikia mashauri yanayowakabili.