SERIKALI YAANZA KULINADI ONYESHO LA SITE SABASABA

Na Aziza Masoud,Dar es Salaam

BODI ya Utalii Tanzania (TTB) imesema maandalizi ya Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Swahili International Tourism Expo (SITE)  yanayotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu yameshaanza na kwamba mpaka sasa  zaidi ya wanunuzi 50 wa huduma za utalii kutoka nchi mbalimbali wameshajisajili.

Akizungumza katika maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF)   Afisa Masoko wa TTB, Abdilahi Ameir, alisema kupitia maonesho hayo SITE imeanzisha dawati la kutoa elimu kuhusu  umuhimu wa maonesho hayo katika sekta ya utalii.

” SITE ni maonesho ya kimataifa yanayowakutanisha wadau wa biashara ya utalii na wanunuzi wa huduma za utalii kutoka mataifa mbalimbali duniani kwa lengo la kukuza biashara na kuitangaza Tanzania kama kitovu cha utalii.

“Mpaka sasa maandalizi ya SITE 2026 yanaendelea vizuri, huku zaidi ya wanunuzi 50 wa huduma za utalii kutoka nchi mbalimbali, ikiwemo Korea, Urusi na nchi za Ulaya Mashariki, wakiwa tayari wamethibitisha ushiriki wao,”alisema Ameir.

Alisema katika maonesho hayo yatakayofanyika jijini Dar es Salam wananchi wa kawaida hawajaachwa nyuma kwani kutakuwa na bustani maalumu ya wanyama pori itakayowapa fursa ya kujifunza na kujionea vivutio vya utalii vilivyopo nchini

Ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki Maonesho ya Swahili International Tourism Expo yatakayofanyika kuanzia Julai 23 hadi 25 katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, ili kujionea fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji katika sekta ya utalii.