Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
Wakazi wa Kigamboni wanatarajiwa kupunguza gharama za uondoshaji wa majitaka baada ya DAWASA kukamilisha ujenzi wa mitambo miwili midogo ya kuchakata majitaka katika Kata za Vijibweni na Gezaulole zenye wakazi zaidi ya 410,400
Mitambo hiyo yenye thamani ya Sh2.3 bilioni imejengwa kwa ajili ya kuchakata majitaka kutoka maeneo hayo, pamoja na kuhudumia magari yanayofanya shughuli za uondoshaji majitaka katika Wilaya ya Kigamboni.

Meneja wa Miradi ya Majitaka DAWASA, Mhandisi Eric Mutalemwa, amesema mitambo hiyo imekamilika, imefanyiwa ukaguzi na sasa iko tayari kuanza kutumika.
“Miradi hii ya Vijibweni na Gezaulole ni ya kisasa ya kuchakata majitaka. Tumekagua na kujiridhisha na ukamilishaji wake na sasa iko tayari kutumika kuhudumia wananchi na watumiaji wa magari ya uondoshaji majitaka katika Wilaya hii,” amesema.

Ameongeza kuwa kukamilika kwa mitambo hiyo kutasaidia kupunguza gharama ambazo wakazi wa Kigamboni na watoa huduma binafsi wamekuwa wakitumia kusafirisha majitaka hadi mabwawa yaliyoko mbali na eneo hilo.
Dereva wa gari la uondoshaji majitaka Kigamboni, Habibu Ally, amesema mradi huo utapunguza gharama za uendeshaji kwa kuwa magari hayatakuwa na ulazima wa kusafirisha majitaka hadi Vingunguti na Kurasini.

“Awali ilitulazimu kwenda hadi katika mabwawa ya majitaka Vingunguti na Kurasini. Umbali huo ulifanya tozo kuwa kubwa kwa wateja na kuongeza gharama za uendeshaji wa magari. Mitambo hii itatusaidia kumwaga majitaka hapa hapa Kigamboni na kutupunguzia gharama,” amesema.
Kukamilika kwa mitambo hiyo kunaongeza uwezo wa huduma za usafi wa mazingira Kigamboni na kupunguza umbali wa usafirishaji wa majitaka kwa wananchi na watoa huduma.



