TOTAL ENERGIES YAZINDUA MPANGO WA KUREJESHA TAKA ZA PLASTIKI

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

KAMPUNI ya TotalEnergies Marketing Tanzania imezindua mpango wa ukusanyaji na uchakataji wa taka za plastiki katika vituo vyake vitano jijini Dar es Salaam, ukiwalenga wananchi kushiriki katika utunzaji wa mazingira huku wakinufaika kupitia mfumo wa pointi.

Mpango huo unaotekelezwa kwa kushirikiana na kampuni ya Arena Recycling Limited, unalenga kuwahamasisha wananchi kutambua kuwa taka za plastiki si uchafu pekee, bali ni rasilimali inayoweza kuchakatwa na kutumika tena kwa manufaa ya kiuchumi na kijamii.

Akizungumza leo Oktoba 1, 2026 wakati wa uzinduzi wa mpango huo, Meneja wa Mauzo wa Total Energies  Tanzania  Thomas Meitaroni alisema kupitia mradi huo wananchi watapata fursa ya kupeleka taka za plastiki katika vituo vilivyoteuliwa, ambapo zitapimwa na washiriki kupewa pointi kulingana na uzito wa taka walizokusanya.

Alisema pointi hizo zitaweza kutumika kupata bidhaa na huduma mbalimbali zinazopatikana katika vituo vya Total Energies, ikiwamo bidhaa za dukani, vilainishi vya magari, huduma za kuosha magari, kubadilisha mafuta ya injini, gesi ya kupikia pamoja na taa za sola.

Alivitaja vituo vitakavyoshiriki katika awamu ya kwanza kuwa ni TotalEnergies Morocco, Azikiwe eneo la Posta, Samora katika Barabara ya Samora na Shekilango, pamoja na kituo cha Mlimani City.

“Tunawalenga wananchi wanaozunguka vituo vyetu kutumia kikamilifu fursa hii kwa kurejesha taka za plastiki, kujikusanyia pointi na wakati huo huo kuchangia katika kupunguza uchafuzi wa mazingira,” alisema Meitaroni.

Alisema taka za plastiki zitakazokusanywa zitasafirishwa, kuchambuliwa na kuchakatwa na baadaye kurejeshwa katika mnyororo wa matumizi kwa kuzalisha bidhaa nyingine zenye manufaa.

“Hatua hiyo, ilielezwa, inalenga kukuza uchumi wa mzunguko, kuboresha usimamizi wa taka na kuongeza manufaa ya kijamii na kiuchumi kwa jamii,”alisema Meitaroni.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Sheria na Uhusiano wa TotalEnergies Tanzania, Getrude Mpangile, amesema mradi huo umetokana na wazo la Arena Recycling na umeungwa mkono kwa kuwa unalenga kuchangia usafi wa mazingira na matumizi bora ya taka za plastiki.

Alisema ushirikiano huo ni sehemu ya juhudi za wadau mbalimbali kushiriki katika kutafuta suluhisho la changamoto ya taka za plastiki na kuendeleza matumizi ya taka kama rasilimali.

Alisema mpango huo unatarajiwa kupanuliwa katika vituo vingine nchini ili kuongeza ushiriki wa wananchi katika uhifadhi wa mazingira na kupunguza kiasi cha taka za plastiki zinazotupwa katika mazingira.

Aidha, TotalEnergies imewataka wateja wake na jamii zinazozunguka vituo vyake kutumia fursa hiyo kwa kushiriki katika ukusanyaji na urejeshaji wa taka za plastiki.

“Tunataka jamii itambue kuwa kila kilo ya plastiki inayokusanywa ni mchango muhimu katika kupunguza uchafuzi wa mazingira, kulinda mifumo ya ikolojia na kujenga jamii yenye uwajibikaji katika usimamizi wa taka,” alisema

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Arena Recycling Limited  Hellena Sailas alisema kampuni hiyo itasimamia ukusanyaji, usafirishaji, uchambuzi na uchakataji wa taka za plastiki zitakazorejeshwa na wananchi kupitia vituo vya TotalEnergies.

Alisema plastiki zitakazokusanywa zitabadilishwa kuwa malighafi kwa ajili ya kutengeneza bidhaa mbalimbali, zikiwamo za ujenzi kama matofali na mbao za plastiki, ambazo zinaweza kutumika kama mbadala wa baadhi ya vifaa vinavyotumika katika ujenzi.

“Kwetu taka ni pesa. Tunataka kuweka thamani katika taka hizi na kuzigeuza kuwa malighafi mpya yenye manufaa kwa jamii na mazingira,” alisema.

Aliongeza kuwa ushirikiano huo ni sehemu ya jitihada za kampuni hiyo kutumia ubunifu na ujasiriamali kutafuta suluhisho la changamoto za mazingira, huku akiishukuru Serikali kwa kuwaunga mkono katika safari yao ya kukuza teknolojia ya uchakataji wa taka.