Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
SERIKALI imesema awamu ya pili ya utekelezaji wa mpango wa bima ya afya itafungua fursa kwa Watanzania wote kujiunga, huku ikisisitiza kuwa utaratibu rasmi wa usajili utatangazwa hivi karibuni.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Emmanuel Tayari alipokuwa akizungumza wakati wa kuzindua huduma za kisaaa za kinywa na meno pamoja na vipandikizi iliyoanzishwa na hospitali ya Aga Khan nchini.

Alisema utekelezaji wa awamu hiyo ya pili utaendelea kwakukamilisha usajili wa kaya maskini, lakini wakati huohuo makundi yote maalumu yatafunguliwa milango ya kujiunga na bima hiyo.
“Katika awamu ya pili tutamalizia kusajili zile kaya maskini, lakini tutafungua kwa makundi yote maalumu. Kwa maana hiyo, Watanzania wote watakuwa wanakaribishwa au kuhamasishwa kujiunga,” alisema Naibu Katibu Mkuu huyo.

Alisema wananchi wanapaswa kusubiri utaratibu rasmi ambao utatangazwa na Serikali hivi karibuni akieleza kuwa hatua hiyo itafanyika muda si mrefu.
Akizungumzia suala la malipo kwa hospitali binafsi zinazotoa huduma kwa wanachama wa bima ya afya, Naibu Katibu Mkuu huyo alisema hakuna changamoto kubwa katika eneo hilo, akieleza kuwa hospitali binafsi zimeendelea kuwa miongoni mwa wanufaika wakubwa wa mfumo wa bima.

Alisema kwa takwimu zilizopo, takribani asilimia 60 ya malipo ya bima ya afya yanaelekezwa katika hospitali binafsi.
“Hospitali binafsi wamekuwa wanufaika wakubwa wa bima ya afya hata kabla ya mfumo huu,kwa hiyo, suala la malipo halina shida,” alisema.
Alitolea mfano Hospitali ya Aga Khan, ambayo hivi karibuni ilisaini mkataba na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuendelea kutoa huduma kwa wanachama wake, akisema hatua hiyo inaonyesha imani iliyopo katika mfumo wa malipo wa bima ya afya.
Akizungumzia kuhusu upanuzi wa huduma za meno alisema kliniki hiyo ya kisasa inaendelea kuongeza ubobevu katika utoaji wa huduma mbalimbali za kibingwa za afya zinazotolewa katika hospitali hiyo iliyopo Dar es Salaam na vituo vyake vya afya nchini.
“Kupitia kliniki hii iloyoboreshwa wagonjwa wanaweza kupata huduma jumuishi za meno katika mazingira ya kisasa,huku huduma hizo zikilenga kusaidia afya ya kinywa,kurejesha utendaji wa meno na kuboresha uzoefu wa jumla wa mgonjwa katika huduma za meno,”alisema.
Alisema uzinduzi wa huduma za kliniki ya meno, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupanua huduma za kibingwa nchini.
Naye Mganga Mkuu wa Hospitali ya Aga Khan Dk. Muzdalifat Abeid alisema hospitali hiyo imeendelea kuwekeza katika huduma za kibingwa, ikiwamo huduma za meno, ili kuwasaidia Watanzania kupata matibabu yenye viwango vya juu bila kulazimika kusafiri nje ya nchi.
Alisema uwekezaji huo unalenga pia kusogeza huduma karibu na jamii, huku huduma hizo zikitolewa kwa viwango vinavyoweza kushindana na huduma zinazopatikana katika nchi nyingine.
“Tumefanya uzinduzi wa dental clinic na huu ni upanuzi mkubwa wa huduma. Tunaendelea kuwekeza kwa sababu huduma hizi sasa zinatolewa pia kwa wanaotumia NHIF,” alisema.
Abeid alisema huduma hizo si idara mpya kabisa, bali ni upanuzi na uboreshaji wa huduma ambazo tayari zilikuwa zikitolewa hospitalini, huku lengo likiwa ni kuunganisha huduma za hospitali na huduma za jamii.
Alisema Aga Khan imekuwa ikifanya kampeni za kutoa elimu kuhusu afya ya kinywa na meno pamoja na programu za uchunguzi katika shule, maeneo ya kazi na jamii.
Kwa mujibu wa Abeid, upanuzi huo utawezesha wananchi kupata huduma za kawaida za meno pamoja na huduma maalumu za kibingwa katika kituo kimoja.
Alisema kwa sasa huduma za kiwango hicho zinapatikana katika vituo vichache nchini, akieleza kuwa hali hiyo imeisukuma Aga Khan kuendelea kuwekeza katika huduma za kibingwa.
“Kwa sababu ya ufinyu wa huduma hizi na kutokuwepo kwa huduma maalumu za kutosha, imetusukuma kuanza na hii. Lakini safari yetu haijaishia hapo; tutaendelea kuwekeza na kufungua huduma nyingine maalumu,” alisema.
Uzinduzi huo unaenda sambamba na mkakati wa kupanua wigo wa huduma za afya nchini, hususan wakati Serikali ikiandaa hatua ya pili ya mpango wa bima ya afya inayotarajiwa kutoa fursa kwa makundi mapana zaidi ya wananchi kujiunga.


