Na Mwandishi Wetu,Pwani
KAMPUNI ya TotalEnergies Marketing Tanzania imeendelea kuimarisha uwekezaji wake nchini baada ya kuzindua kituo chake cha 125 cha mafuta kilichopo Kibaha mkoani Pwani, hatua inayolenga kusogeza huduma za nishati karibu na wananchi, kuongeza ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Uzinduzi huo unaashiria dhamira ya kampuni hiyo ya kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya vituo vya mafuta nchini kupitia mfumo wa Company-Owned Dealer-Operated (CODO) unaowawezesha wawekezaji wazawa kushirikiana na kampuni katika kuendesha biashara huku wakitoa huduma zenye viwango vya kimataifa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi, Mkurugenzi Mtendaji wa TotalEnergies Marketing Tanzania, Mamadou Ngom, alisema kufunguliwa kwa kituo hicho kunaonesha imani kubwa ambayo kampuni hiyo inaendelea kuwa nayo kwa Tanzania kama eneo salama la uwekezaji.
Alisema kituo hicho, ambacho ni cha 125 katika mtandao wa TotalEnergies nchini, kitaleta huduma za mafuta, vilainishi, gesi na suluhisho nyingine za nishati kwa ubora, huku kikitoa fursa zaidi za ajira na biashara kwa wananchi.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kibaha, Moses Magogwa, alisema Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji kwa kutenga maeneo zaidi ya uwekezaji ili kuongeza ajira, mapato na kukuza uchumi wa Mkoa wa Pwani.
Alieleza kuwa uwekezaji huo unabadilisha taswira ya Wilaya ya Kibaha na kuifanya kuwa kitovu muhimu cha biashara kutokana na ongezeko la huduma za kisasa zinazokidhi mahitaji ya wakazi na wasafiri wanaotumia barabara kuu ya Dar es Salaam kuelekea mikoa ya ndani.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Fortes Energy Ltd, Flavianus Momba, alisema ushirikiano kati ya sekta binafsi na TotalEnergies umefungua fursa mpya za uwekezaji na maendeleo ya biashara katika eneo hilo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sheria na Mawasiliano wa TotalEnergies Tanzania, Getruda Pangile, alisema kampuni itaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha huduma za nishati zinawafikia wananchi kwa ubora, usalama na kwa kuzingatia maendeleo endelevu.

Mwendeshaji wa Kituo cha TotalEnergies Kibaha, Naftal Philip, alisema kituo hicho tayari kimeanza kupokea wateja wengi na kimejipanga kutoa huduma bora kwa kutumia bidhaa zenye ubora wa kimataifa pamoja na mifumo ya kisasa ya malipo.
Mbali na huduma za mafuta aina ya Excellium, vilainishi na gesi, kampuni hiyo imesema katika kipindi kijacho kituo hicho kitakuwa na duka la Bonjour, karakana ya huduma za magari pamoja na migahawa ya chakula cha haraka ili kukifanya kuwa kituo cha huduma zote kwa wasafiri na wakazi wa eneo hilo.

TotalEnergies imekuwa ikifanya shughuli zake nchini Tanzania tangu mwaka 1969, ikijihusisha na usambazaji wa mafuta, gesi ya LPG, vilainishi pamoja na suluhisho za nishati jadidifu ikiwemo miradi ya umeme wa jua kupitia mpango wa Access to Solar.
Uzinduzi wa kituo hicho unaongeza idadi ya vituo vya TotalEnergies nchini kufikia 125 na unaendelea kuthibitisha mchango wa kampuni hiyo katika kukuza uchumi, kuongeza ajira na kuimarisha upatikanaji wa huduma za nishati kwa Watanzania.


