Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imemkamata raia wa Kenya, Kilonzo Mwende (35) na gramu 131 za heroin ambapo mtuhumiwa huyo alikuwa akiishi nchini tangu mwaka 2023 akijifanya mfanyabiashara wa kuuza chai ya maziwa katika ofisi mbalimbali.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Januari 8, 2026 Kamishina Jenerali wa DCEA Aretas Lyimo amesema mtuhumiwa huyo na wengine wamekamatwa katika operesheni ya mwezi Desemba ambapo walikamata kiasi kikubwa cha dawa za kulevya chenye uzito wa zaidi ya kilogramu 9,683.89 katika mikoa mbalimbali huku wengine wakiwa wameshafikishwa katika vyombo vya sheria.

Amesema Kilonzo Mwende alikamatwa katika mtaa wa Bustani, Sinza, akiwa na gramu 131 za heroin huku uchunguzi umebaini kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa akiishi nchini tangu mwaka 2023 akijifanya mfanyabiashara wa kuuza chai ya maziwa katika ofisi mbalimbali huku akitumia shughuli hiyo kama kiini macho cha kusambaza dawa za kulevya.
“Raia huyu wa Kenya amekiri kuanza kuingiza dawa za kulevya kidogo kidogo baada ya kubaini upungufu wa dawa hizo nchini, akizisambaza katika maeneo mbalimbali ya jiji ili kujipatia kipato, hivyo tunatoa wito kwa wananchi kutoa taarifa kuhusu wageni au biashara zinazotia shaka katika maeneo yao kupitia namba maalum ya dharura 119,”amesema Kamishna Lyimo.

Mbali na Mkenya Katika operesheni nyingine, watu watatu wamekamatwa wakiwa wanasafirisha bangi yenye uzito wa zaidi ya kilogramu 1,893 kutoka mkoani Morogoro kwenda Dar es Salaam, huku mamlaka ikionya pia kuhusu matumizi ya baadhi ya watumishi wa serikali kama vichaka vya kupitisha dawa hizo kwa kutumia vitambulisho vya kazi.
Aidha, katika ukaguzi wa kampuni za usafirishaji mizigo jijini Dar es Salaam, amesema pakiti za mirungi zenye uzito wa kilogramu 9.54 zilikamatwa zikiwa zimefichwa na kusomeshwa kama majani ya mwarobaini, zikitokea nchini Kenya, huku operesheni zilizofanyika katika mikoa mbalimbali zikikamata heroin, bangi na mirungi kwa kiasi kikubwa pamoja na kuteketeza hekari 14 za mashamba ya bangi.
“Mamlaka inasisitiza kuwa itaendelea kuimarisha operesheni hadi ngazi ya wilaya na vijiji, kudhibiti uzalishaji na usafirishaji wa bangi na mirungi, na kuwataka wananchi kuendelea kushirikiana kwa kutoa taarifa ili kuvunja na kumaliza kabisa mitandao ya biashara ya dawa za kulevya nchini Tanzania”,Amesema Kamishna Jenerali Lyimo.


