UDOM, WIZARA YA KATIBA NA SHERIA, LSF WASHIRIKIANA KUIMARISHA HUDUMA ZA MSAADA WA KISHERIA

Na Asha Mwakyonde, DODOMA

WIZARA ya Katiba na Sheria imesaini mkataba wa makubaliano na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) pamoja na Shirika la Legal Services Facility (LSF), kwa lengo la kupanua na kuimarisha huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi ili waweze kupata haki zao kwa urahisi zaidi.

Kupitia makubaliano hayo, Chuo Kikuu cha Dodoma kitaanzisha Kituo cha Msaada wa Kisheria katika Mkoa wa Dodoma kitakachotoa huduma za kisheria kwa wananchi wa mkoa huo.

Aidha, kituo hicho kitafanya tafiti mbalimbali kuhusu migogoro ya kisheria inayowakabili wananchi katika maeneo tofauti nchini, hatua itakayosaidia kubaini changamoto na kupendekeza suluhu zake.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi, amesema ushirikiano huo ni sehemu ya utekelezaji wa kampeni ya Mama Samia Legal Aid, inayolenga kusogeza huduma za kisheria karibu zaidi na wananchi, hususan wale wasio na uwezo wa kuzimudu.

Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma anayesimamia Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi, Profesa Razack Bakari, amesema makubaliano hayo yataongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi wengi zaidi, sambamba na kuimarisha tafiti na elimu ya sheria kwa jamii.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Legal Services Facility (LSF), Lulu Ng’wanakilala, amesema kuwa upatikanaji wa haki ni haki ya kikatiba na msingi muhimu wa utawala bora, hivyo ushirikiano huo utachangia kuongeza ufanisi na usawa katika utoaji wa huduma za kisheria nchini.