Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
WAZIRI wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema kukamilika kwa ujenzi wa eneo la kuhifadhi kontena lenye sqm 200000 kutaongeza ufanisi kutoka kupokea kontena 8000 hadi 13,000 kwa mwaka.
Akizungumza Januari 9 , 2026 katika eneo hilo lililopo Kurasini ambapo amefanya ziara yakuangalia utendaji kazi wa bandari Profesa Mbarawa alisema ujenzi wa eneo hilo ambao unafanywa na serikali kwakushirikiana na mwekezaji ni muendelezo wa maboresho ya bandari yenye lengo la kuongeza ufanisi.

“Nimekuja kutembelea,nimetoka kuangalia eneo la Terminal 2 lakini pia nimekuja katika eneo la pili Kurasini kuangalia hatua tuliyofikia katika eneo hili lakuhifadhi makontena,eneo hili linajengwa na mwekezaji lina sqm 200000 maalum kwakuhifadhia makontena,mizigo yote itakuwa inahifadhiwa hapa baada yakushuka kwenye meli,”alisema Profesa Mbarawa.
Alisema kukamilika kwa ujenzi wa eneo hilo utaongeza ufanisi wa bandari katika kihifadhi mizigo ambapo itakuwa na uwezo wakupokea 13,000 kutoka 8000 za sasa.

Alisema mpaka sasa kazi ya ujenzi wa eneo hilo umefikia asilimia 90 ambapo inatarajiwa kukamilka mwishoni mwa mwezi Februari.
“Kwa sababu tumekubaliana kukamilisha mwishoni mwa mwezi huu kwa sasa kila wiki tutakuwa tunakuja kukagua,naamini baada ya kukamilika kwa ujenzi huu mwaka mmoja mizigo itaongezeka kwa asilimia mia,”alisema Profesa Mbarawa.
Alisema ongezeko la mizigo litaambatana na mikakati yakutanua maeneo yakuhifadhi zikiwemo uboreshaji wa miundombinu yakuelekea bandari Kavu ya Kwala pamoja na bandari nyingine.

“Tukifanya mikakati yote hii itatusaidia bandari yetu ipumue,mikakati yote hii ina lengo la kuhakikisha tunafungua bandari ajira zinakuja na kukuza uchumi “alisema Profesa Mbarawa.
Akizungumzia ukusanyaji wa mapato ya bandari alisema kwa sasa makusanyo yamefikia Sh Trilioni mbili tofauti na awali ambayo yalikuwa Sh Bilioni 700.

Awali Mkurugenzi wa Bandari Dar es Salaam Abeid Gallus alisema ufanisi ufanisi wa bandari umeongezeka ambapo mwaka 2024 walihudumia kontena 18,000 lakini mwaka 2025 zimeongezeka na kufikia kontena 36,000.
“Makusanyo awali ilikuqa Sh Bilioni 700 mpaka 800 sasa imefika Sh Trilioni mbili,uwekezaji huu unaofanyika bandarini ni muhimu na tutaendelea kuweka mazingira mazuri miundombinu wezeshi kuhakikisha bandari inafunguka,’alisema Gallus.


