Na Mwandishi Wetu,Tanga
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwigulu Nchemba, amekagua na kuweka jiwe la msingi la Mradi wa Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha kilovolti 132/33 katika eneo la Mkata, wilayani Handeni, mkoani Tanga.
Mradi huo uliogharimu Shilingi bilioni 44 unahusisha ujenzi wa vituo viwili vya kusambaza umeme pamoja na ufungaji wa transfoma mbili zenye uwezo wa MVA 60 kila moja, ambazo zitapooza umeme kutoka kilovolti 132 hadi kilovolti 33 kwa ajili ya matumizi ya wananchi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, alimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha zilizosaidia kukamilisha mradi huo.
“Kabla ya mradi huu, umeme unaopatikana katika wilaya ya Handeni na Kilindi ulikuwa unatokea Tanga Mjini. Lakini mradi huu utakapokamilika Novemba mwaka huu, umeme utatokea Chalinze, utakuja kupoozwa hapa Mkata, na hatimaye kuwafikia wananchi wa wilaya ya Handeni na Kilindi kwa uhakika zaidi,” amesema Ndejembi.


Amefafanua kuwa kupitia miundombinu hiyo mipya, umeme utasafirishwa kutoka Mkata kwenda Msisi kwa umbali wa zaidi ya kilomita 45, hatua itakayoongeza uwezo wa usambazaji na kuimarisha huduma katika maeneo hayo.
Ndejembi ameongeza kuwa uwepo wa kituo hicho utaboreshesha hali ya upatikanaji wa umeme na kurahisisha shughuli mbalimbali wilayani humo ikiwemo uchimbaji wa madini, viwanda, kilimo na biashara,” jambo litakalochochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi wa Handeni na Kilindi.



