Na Mwandishi Wetu, Singida
WAKALA wa Nishati Vijijini imeanza utekelezaji wa mpango mkakati wa kitaifa wa nishati safi ya kupikia ili kufikia lengo la zaidi ya asilimia themanini 80% ya watanzania ifikapo mwaka 2034 wawe wanatumia nishati safi ya kupikia nishati ambayo ni salama kwa mtumiaji na rafiki kwa mazingira.
Akizungumza wakati wa ugawaji wa majiko katika Kata na Tarafa ya Irongero katika Wilaya ya Singida leo tarehe 24 Februari 2026 Mhandisi wa miradi ya REA Mkoani Singida, Mha.Nathan Msanze amesema kuwa Wakala ya Nishati Vijijini-REA katika mkoa huo umeanza usambazaji wa majiko banifu 6,692.

Amesema kuwa majiko hayo yatagawiwa kwa wananchi kwa bei ya ruzuku katika wilaya zote na Halmashauri za mkoa huo ambazo ni Ikungi majiko 1,116, Iramba 1,116, Itigi 1,115, Manyoni 1,115, Mkalama 1,115 na Singida 1,115.
Mhandisi Nathan amesema kuwa mradi huo unahusisha usambazaji wa majiko banifu yanayotumia kuni na mkaa kidogo ili kupunguza matumizi ya vyanzo hivyo vya nishati pamoja na athari za moshi zitokanazo na matumizi katika majiko ya kawaida. Katika mkakati huo Wakala wa Nishati Vijijini umeandaa mpango wa uuzwaji wa majiko banifu 200,000 kwa bei ya ruzuku yenye ufanisi mkubwa katika utumiaji wake.

Amesema kuwa mikataba hiyo ilisainiwa tarehe 9 Mei , 2025 na itatekelezwa ndani ya miezi 15. Gharama ya mradi ni TZS 340,288,200 kwa mkoa wa Singida na ruzuku inayotolewa na Wakala wa Nishati Vijijini ni TZS 289,230,508.47 sawa na asilimia 85 ya gharama ya mradi. Wananchi wanachangia TZS 51,057,691.53 sawa na asilimia 15 ya gharama ya mradi.
Mtoa huduma ni Tango Energy Limited ambapo jumla ya majiko banifu 6,692 yatauzwa kwa wananchi kwa bei ya ruzuku. Gharama ya jiko moja ni TZS 50,847.46 lakini serikali imetoa ruzuku ya asilimia 85 hivyo mwananchi atanunua kwa gharama ya TZS 7,600.

Kwa upande wao wananchi ambao wamenufaika na majiko hayo katika kata ya Ilongero wakiongozwa na Diwani wa Kata hiyo Mhe Issa Mwiru kwa kauli moja wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuamua kutoa majiko bunifu kwa bei ya ruzuku ambayo itawanufaisha wananchi wote.



