KAMATI YA BUNGE YAITAKA SERIKALI KUONGEZA BAJETI YA VIWANDA

Na Asha Mwakyonde, DODOMA

KATIKA kipindi ambacho Tanzania inaelekea kwenye mageuzi makubwa ya kiuchumi kupitia Dira ya Taifa 2050, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imeibuka na mapendekezo mazito yanayolenga kuimarisha sekta ya viwanda, biashara na uwekezaji nchini.

Kamati hiyo imeitaka Serikali kuongeza bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na kuharakisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa taifa.

Akisoma taarifa ya kamati ya kudumu ya bunge ya viwanda, biashara, kilimo na mifugo kuhusu utekelezaji wa majukumu ya wizara ya viwanda na biashara kwa mwaka wa fedha 2025/2026 pamoja na maoni ya kamati kuhusu makadirio ya mapato na matumizi y kwa mwaka wa fedha bungeni leo Mei 22, 2026 bungeni jijini hapa D Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mariam Ditopile.

Amesema sekta ya viwanda imepewa nafasi kubwa katika Dira ya Taifa 2050 hivyo kuna umuhimu mkubwa wa Serikali kuongeza fedha kwa Wizara hiyo ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuleta mageuzi ya kweli ya kiuchumi.

Ditopile amesema Kamati imebaini changamoto ya upatikanaji wa fedha za maendeleo kwa wakati, hali inayosababisha baadhi ya miradi kusuasua au kutotekelezwa kabisa licha ya kuidhinishiwa fedha na Bunge. Kutokana na hali hiyo, Kamati imeishauri Serikali kuhakikisha fedha za miradi zinatolewa kwa wakati na kwa kiwango kilichopangwa.

Aidha kwa mujibu wa Ditopile, Kamati imeeleza kutoridhishwa na kuchelewa kukamilika kwa miradi ya Liganga na Mchuchuma pamoja na mradi wa Magadi Soda Engaruka, ikisema hali hiyo inaendelea kuifanya nchi kutegemea bidhaa kutoka nje ikiwemo chuma, kemikali na malighafi nyingine muhimu kwa maendeleo ya viwanda.

“Miradi hii ni muhimu katika kuongeza ajira, kukuza uchumi wa viwanda na kutumia rasilimali za taifa kwa maendeleo ya wananchi, hivyo Serikali inapaswa kuchukua hatua za haraka kuhakikisha inaanza kutekelezwa,” amesema Ditopile.

Katika hatua nyingine, Kamati imeishauri Serikali kuharakisha uanzishwaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Viwanda nchini, ikieleza kuwa kutokuwepo kwa mfuko huo kunaathiri ukuaji wa sekta ya viwanda na uchumi kwa ujumla. Kamati pia imependekeza taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo kuchangia fedha katika mfuko huo ili kuongeza mtaji wake.

Ameeleza kuwa Kamati imeitaka Serikali kufanya tathmini ya kina kuhusu tozo mbalimbali za biashara ambazo zimekuwa zikiongeza gharama za uzalishaji na kudhoofisha ushindani wa bidhaa za ndani dhidi ya bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi.

Katika sekta ya huduma za mawasiliano, ameongeza kuwa Kamati imeeleza kuwepo kwa malalamiko ya wananchi kuhusu thamani halisi ya muda wa maongezi na bando za intaneti.

Amefafanua kuwa imeishauri Wizara kupitia Wakala wa Vipimo (WMA) kuanza kuhakiki vipimo vinavyotumika katika huduma hizo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma wanazolipia kwa usahihi.

“Kamati imeitaka Wizara ya Viwanda na Biashara kushirikiana na Wizara ya Nishati kuhakikisha mita zote mpya za umeme zinahakikiwa na Wakala wa Vipimo kabla ya kusimikwa kwa watumiaji ili kuondoa malalamiko yanayotokana na bili zisizo sahihi,” amesema.

Akizungumzia kuhusu biashara ya lumbesa, amesema Kamati imeeleza kuwa bado ni changamoto kubwa inayowakandamiza wakulima na kuikosesha Serikali mapato, hivyo imependekeza ushirikiano wa pamoja kati ya mamlaka mbalimbali za udhibiti wa vipimo ili kupata suluhu ya kudumu.

“Kamati imeonya juu ya kuendelea kuwepo kwa bidhaa feki sokoni, ikisema hali hiyo inaathiri uwekezaji, usalama wa watumiaji na mapato ya Serikali. Imeshauri kuongezwa kwa ukaguzi mipakani na sokoni pamoja na kuzipatia mamlaka husika rasilimali watu na fedha za kutosha,” ameeleza.

Katika hatua nyingine, ameeleza kuwa Kamati imeitaka Serikali kuhakikisha mifumo ya Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Wizara ya Kilimo inasomana ili kurahisisha ufuatiliaji wa mnyororo wa uzalishaji, usindikaji na biashara ya mazao ndani na nje ya nchi.

Pia imeeleza wasiwasi wake kuhusu biashara ndogo ndogo zinazofanywa na baadhi ya raia wa kigeni nchini, hali inayodaiwa kuathiri wafanyabiashara wazawa pamoja na kupunguza nafasi za ajira na kujiajiri kwa wananchi.

Makamu Mwenyekiti huyo amefanunua kuwa Sambamba na hayo, Kamati imezungumzia changamoto ya uhaba wa hosteli katika Vyuo vya Elimu ya Biashara (CBE), ikibainisha kuwa asilimia 3.57 pekee ya wanafunzi ndiyo wanaopata nafasi ya kuishi hostelini.

Aidha Kamati imeitaka Serikali kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa hosteli zaidi ili kupunguza changamoto zinazowakabili wanafunzi, hususan wa kike, wanaoishi nje ya vyuo.