๐Vituo 50 kujengwa nchini
๐Wateja milioni moja kunufaika na majiko ya umeme
Na Mwandishi Wetu,Dodoma
Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, leo Juni 11, 2026 jijini Dodoma amezindua rasmi mpango wa ukopeshaji wa majiko ya umeme kwa wateja wa TANESCO pamoja na mradi wa vituo vya kuchajia vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme, hatua inayolenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Ndejembi amesema matukio hayo mawili ni ya kihistoria kwa kuwa yanafungua ukurasa mpya wa matumizi ya umeme nchini, si kwa ajili ya mwanga pekee bali pia kama nyenzo ya kuboresha maisha ya wananchi, kupunguza gharama za maisha na kulinda mazingira.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya nishati, hali iliyowezesha uzalishaji wa umeme nchini kufikia zaidi ya megawati 4,000 na kuifanya Tanzania kuwa na umeme wa kutosha kwa matumizi mbalimbali ya maendeleo.
Kuhusu mpango wa majiko ya umeme, Waziri Ndejembi amesema wananchi sasa wataweza kupata majiko yaliyo sanifu kwa mkopo na kulipa gharama hizo kidogo kidogo kupitia manunuzi yao ya umeme wa LUKU. Amesema hatua hiyo itaondoa kikwazo cha gharama za awali za ununuzi wa majiko hayo na kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Ameeleza kuwa mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024โ2034 unaolenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, huku asilimia 20 wakitumia umeme kwa shughuli za kupika.
Waziri Ndejembi amesema matumizi ya kuni na mkaa yameendelea kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira, ambapo zaidi ya hekta 469,000 za misitu hupotea kila mwaka. Amesisitiza umuhimu wa kuimarisha matumizi ya nishati mbadala na safi ili kulinda mazingira na afya za wananchi.
Katika sekta ya usafiri, TANESCO imezindua kituo chake cha kwanza cha kuchajia vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme na kuanza rasmi utekelezaji wa mradi wa kufunga vituo vya kuchajia katika ofisi zake za mikoa mbalimbali nchini ili kurahisisha matumizi ya magari, pikipiki na bajaji za umeme.
Amesema mradi huo umewezeshwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa kushirikiana na kampuni ya AUTEL, ambayo imetoa mashine 50 za kisasa za kuchajia magari ya umeme zitakazofungwa katika ofisi za TANESCO kote Nchini.
Aidha, Waziri Ndejembi ameipongeza TANESCO kwa ubunifu huo na kusisitiza kuwa matumizi ya umeme katika kupikia na usafiri ni sehemu ya mapinduzi ya nishati safi yatakayochochea ukuaji wa uchumi, kuboresha maisha ya wananchi na kuiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya ushindani katika uchumi wa kijani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, amesema kupitia mradi huo uliozinduliwa vituo 50 vya kuchajia vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme vitajengwa katika Mikoa yote Nchini katika Ofisi za TANESCO.
Ameongeza kuwa wateja takribani milioni moja wanaopata huduma ya umeme kupitia taasisi hiyo wanatarajiwa kunufaika na mpango wa kupata majiko ya umeme kwa mkopo.


