MIRADI YA UMWAGILIAJI KUONGEZA UZALISHAJI AJIRA KWA VIJANA

Na  Aziza Masoud, Dodoma

SERIKALI imeendelea kuwekeza katika miradi ya umwagiliaji kwa lengo la kuwawezesha wakulima kupata maji ya uhakika kwa ajili ya uzalishaji wa mazao ya chakula, mboga mboga na matunda kwa lengo la kuongeza tija na kuimarisha kipato  kwa wananchi.

Akizungumza leo Agosti 3, 2026 jijini Dodoma katika Maonesho ya Wakulima ya Kimataifa  Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa Umwagiliaji (NIRC) Raymond Mndolwa  alisema katika kipindi cha miaka mitatu, utekelezaji wa miradi hiyo imewezesha wakulima katika maeneo mbalimbali kupata maji kutoka kwenye mito na mabonde kwa ajili ya shughuli za kilimo, huku juhudi zikielekezwa pia katika kuhakikisha maeneo yenye fursa za kilimo yanaendelezwa kwa miundombinu ya umwagiliaji.

Alisema utekelezaji wa miradi hiyo ni hatua  muhimu katika kuwawezesha wakulima kuongeza uzalishaji na kutumia fursa zilizopo katika maeneo yao.

“Pamoja na kuwawezesha wakulima, miradi ya umwagiliaji inatarajiwa kufungua fursa zaidi za ajira kwa vijana, hususan katika usimamizi na uendeshaji wa miundombinu ya umwagiliaji.

“Vijana wenye ujuzi katika masuala ya umwagiliaji watawezeshwa kushiriki katika usimamizi wa miradi hiyo, ikiwemo shughuli za uendeshaji wa visima, ufungaji na matengenezo ya mifumo ya umwagiliaji,”alisema Mndolwa.

Alisema matarajio ya tume ndani ya miaka mitatu ijayo miradi hiyo itaweza kutoa ajira kwa vijana wengi, hatua itakayosaidia kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira na kuongeza ushiriki wa vijana katika sekta ya kilimo.

Alisema mipango hiyo inaendana na jitihada za Serikali za kuwawezesha vijana kutumia sekta ya kilimo kama chanzo cha ajira na kipato, huku uwekezaji katika umwagiliaji ukipewa kipaumbele ili kuhakikisha kilimo kinafanyika kwa tija na kwa uhakika zaidi.

Alisisitiza kuwa kwa  kuendelea kuendeleza miradi ya umwagiliaji katika halmashauri mbalimbali, wakulima wataweza kuzalisha kwa misimu mingi zaidi na kuongeza upatikanaji wa mazao ya chakula na biashara.

Hatua hiyo pia inatarajiwa kuchochea shughuli nyingine za kiuchumi katika maeneo yanayozunguka miradi ya umwagiliaji, ikiwemo biashara ya pembejeo, usafirishaji na masoko ya mazao.