TTCL: UHIFADHI WA TAARIFA NDANI YA NCHI UIMARISHA USALAMA KIDIGITALI

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

SHIRIKA  la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limesema kuhifadhi taarifa na mifumo ya taasisi ndani ya nchi kupitia Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Taarifa Kidijitali (National Internet Data Centre – NIDC) ni hatua muhimu ya kuimarisha usalama wa taarifa na kulinda uhuru wa kidijitali wa Tanzania.

Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Mtaalamu wa TEHAMA wa TTCL Data Centre, Alfred Thawe, alisema huduma za Cloud zinazotolewa na kituo hicho zimebuniwa kuwezesha wananchi, taasisi, wafanyabiashara na wanafunzi kuhifadhi taarifa zao kwa usalama bila kulazimika kutumia seva zilizopo nje ya nchi.

Alisema huduma hizo zinajumuisha uhifadhi wa taarifa (Storage as a Service), uendeshaji wa mifumo mbalimbali (Infrastructure as a Service), usajili wa vikoa na huduma nyingine za kidijitali zinazowezesha watumiaji kusimamia taarifa zao kwa urahisi na kwa gharama nafuu.

“Faida kubwa ya huduma hizi ni kwamba taarifa zote zinabaki kuhifadhiwa ndani ya Tanzania, jambo linaloongeza usalama wa taarifa, kulinda faragha za watumiaji na kuimarisha uhuru wa kidijitali wa taifa,” alisema Thawe.

Alisema TTCL Data Centre imefikia kiwango cha kimataifa cha Tier III, kinachoonyesha ubora wa miundombinu ya kituo hicho katika utoaji wa huduma za kuhifadhi taarifa na mifumo ya TEHAMA.

Alieleza kuwa huduma hizo zinapatikana kwa wananchi wote, wakiwemo wanafunzi, wajasiriamali, kampuni na taasisi mbalimbali, ambapo usajili hufanyika kupitia mfumo wa NIDC kwa kutumia taarifa za msingi kama jina na barua pepe.

Alisema ushiriki wa TTCL katika Maonesho ya Nanenane unalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu matumizi ya teknolojia za kidijitali na mchango wake katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku akiwakaribisha kutembelea banda la TTCL kupata elimu na kujiunga na huduma hizo.