WATANZANIA WATAKIWA KUONGEZA KASI YA KUNYWA CHAI

Na Aziza Masoud, Dodoma

BODI ya Chai nchini imesema  asilimia 10 pekee ya watanzania wanakunywa chai nchini  na kwamba asllimia kubwa inayobaki inapelekwa nje.

Akizungumza katika Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima Nane nane,Afisa Mkuu wa Mipango na Uhamasishaji wa Bodi ya Chai Tanzania, Godlove Myinga, alisema asilimia 10 pekee ya chai inayozalishwa nchini ndiyo inayotumiwa na Watanzania, huku asilimia kubwa ikipelekwa katika masoko ya nje kutokana na ubora wake na kukidhi viwango vya kimataifa.

Alisema  kutokana na hali hiyo, bodi imeanza kampeni ya kuhamasisha wananchi kuongeza matumizi ya chai pamoja na kuwekeza katika mnyororo wa thamani wa zao hilo ili kuongeza mchango wake katika uchumi wa taifa.

“Licha ya Tanzania kuzalisha chai yenye ubora wa kimataifa, matumizi ya ndani bado ni madogo,sehemu kubwa ya chai inayozalishwa husafirishwa kwenda masoko ya Ulaya, Marekani na Asia kutokana na ubora wake, huku Watanzania wengi wakikosa fursa ya kunufaika na faida zake kiafya.

“Chai ina faida nyingi ikiwemo kusaidia kuondoa sumu mwilini, kuimarisha afya ya figo, kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo, kuboresha afya ya kinywa na meno pamoja na kuwa na kemikali asilia za polyphenols zinazosaidia kulinda mwili dhidi ya magonjwa mbalimbali,” alisema  Myinga.

Alisema kuwa matumizi ya chai pia husaidia kupunguza uchovu wa akili na kuleta utulivu, hivyo wananchi wanapaswa kujenga utamaduni wa kunywa chai mara kwa mara.

Mbali na matumizi, Myinga alisema sekta ya chai ina fursa nyingi za uwekezaji zikiwemo kilimo cha chai, uanzishaji wa viwanda vya kuchakata chai, biashara ya kuchanganya na kufungasha chai pamoja na masoko ya ndani na nje ya nchi.

Alieleza kuwa sababu kubwa ya matumizi madogo ya chai nchini ni uelewa mdogo kuhusu faida zake, jambo ambalo limeifanya Bodi ya Chai kuendelea kutoa elimu kupitia maonesho ya Sabasaba, Nanenane, vyombo vya habari na majukwaa mbalimbali ya umma.

Aidha, alisema Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza Afrika Mashariki kuanza kulima chai mwaka 1892 baada ya zao hilo kuanzia nchini China, ambako awali lilitumika kama dawa kabla ya kusambaa duniani.

Alisisitiza kuwa kuongezeka kwa matumizi ya chai ya Tanzania kutachangia kuboresha afya za wananchi, kuongeza soko la ndani na kuimarisha mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa nchi.