Na Mwandishi Wetu,Dodoma
CHUO Cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kimesema muitikio wa wanawake katika fani ya ubaharia kwa sasa umekuwa mkubwa tofauti na zamani ambapo iliaminika kuwa kazi hiyo ni ya kihuni.
Akizungumza Agosti 4, 2026 katika Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima Nanenane Mkufunzi Msaidizi wa DMI Jacquline Lema alisema kuwa pamoja na wanafunzi kuwa na muitikio mkubwa katika fani mbalimbali zilizopo katika sekta ya bahari kwa upande wa wanawake muitikio ni mkubwa zaidi ukilinganisha na miaka ya nyuma.

“Upande wa wanawake muitikio ni mkubwa ukilinganisha na miaka mitatu minne nyuma idadi ya wanawake wanaokuja kusoma pale chuoni hususani kozi za ubaharia ni wengi,wengi wamepata elimu na kufahamu ubaharia sio kazi ya wanaume pekee .
“Wamefahamu ubaharia sio kazi ya kihuni ni taaluma kama ilivyo taaluma nyingine kwa hiyo wanakuja wanapata mafunzo chuoni kwetu wanaenda kufanya kazi melini na kwenye taasisi nyingine ambazo wanaajirika,”alisema Lema ambaye pia ni baharia.

Alisema pamoja na muitikio huo lakini katika fani ya ubaharia wanawake bado wachache hivyo amewashauri mabinti kusoma ubaharia kwakuwa hatopoteza muda kutokana na uhitaji uliopo katika tasnia hiyo hasa katika meli.
Akizungumzia kuhusu kasi ya wanafunzi kujiunga na chuo hicho amesema ni kubwa na kwamba bado wanaendelea kujitangaza ili kuongeza idadi zaidi.

“Mapokeo ya wanafunzi ni mkubwa chuo chetu kinaendelea kujitangaza idadi ya wanafunzi inaongezeka mwaka hadi mwaka,kwa mfano kwa mwaka 2025 waliweza kuhitimu zaidi ya wanafunzi 2000 katika fani mbalimbali,”alisema Lema.
Alisema kupitia kozi wanazotoa wanazalisha rasilimali watu wanaoenda kufanya kazi baharini,mafundi wa uhandisi,manahodha pamoja na watalaam wengine wanaoenda kufanya kazi katika sekta za mafuta na gesi.

Aliwataka wanachi kufika katika banda la DMI lililopo ndani ya banda la Wizara ya Uchukuzi ili kuweza kupata ufafanuzi zaidi kuhusu sekta ya bahari hasa kipindi hiki ambacho nchi imejielekeza katika kukuza uchumi wa buluu.


