CHAVUA YA NYUKI YATAJWA KUWA NA  FAIDA KIAFYA

Na Aziza Masoud, Dodoma

WAKATI asali ikiendelea kuwa zao la nyuki linalofahamika na kutumiwa na Watanzania wengi, wazalishaji wa mazao ya nyuki wameanza kuhamasisha matumizi ya chavua ya nyuki (bee pollen), wakisema bado haijapata soko kubwa licha ya kuwa na virutubisho vinavyoweza kusaidia afya.

Akizungumza katika banda la  Benki ya Kilimo Tanzania (TADB)  katika Maonesho ya Wakulima Taifa  Nane nane,Mkurugenzi wa Kampuni ya Triple D Farms Supply, Deogratias Kambalile, alisema chavua ni miongoni mwa mazao ya nyuki ambayo bado ni mapya katika soko la Tanzania, jambo linalochangia kutofahamika kwake kwa watumiaji wengi.

Alisema chavua ina virutubisho mbalimbali ikiwemo vitamini B, C, madini na amino asidi ambavyo vina umuhimu katika mwili wa binadamu.

“Chavua inaweza kusaidia kuongeza virutubisho mwilini, kuimarisha mfumo wa kinga, afya ya ngozi, moyo na mifupa kutokana na madini yaliyomo ndani yake,” alisema Kambalile.

Alifafanua kuwa chavua inaweza kutumiwa kwa kuchanganywa na maji, juisi au chai, huku akisisitiza watumiaji kufuata kiasi kinachoshauriwa.

Kambalile alisema kampuni hiyo inazalisha zaidi ya mazao nane yanayotokana na nyuki, lakini chavua ndiyo bidhaa mpya inayohitaji kupewa elimu zaidi kwa wananchi ili kuongeza matumizi yake.

Kwa sasa alisema bidhaa hiyo inapatikana zaidi Dar es Salaam na Singida, huku juhudi zikiendelea kupanua masoko katika maeneo mengine nchini.

Alisema uelewa mdogo wa wananchi kuhusu chavua umechangia bidhaa hiyo kutopenya kwa kasi sokoni, tofauti na asali ambayo tayari imejijengea soko kwa muda mrefu.