DAWASA YAJA NA SULUHISHO HUDUMA YA MAJI MKURANGA

Na Mwandishi Wetu,Pwani
‎
‎Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imenunua pampu mpya yenye thamani ya Sh milioni 250 kwa ajili ya kisima kinachohudumia Mkuranga Mjini, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji na kuondoa changamoto ya mgao wa maji katika eneo hilo.
‎
‎Pampu hiyo inatarajiwa kufungwa na kuanza kufanya kazi Mwezi Oktoba mwaka huu, huku hatua hiyo ikitarajiwa kuboresha upatikanaji wa maji kwa wananchi wa Mkuranga Mjini wapatao 67,000.

‎
‎Hatua hiyo imepongezwa na Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Jimbo la Mkuranga Mheshimiwa Abdallah Ulega aliyesema ukuaji wa kasi wa Mji wa Mkuranga umeongeza mahitaji ya huduma ya maji, hivyo hatua za DAWASA ni muhimu katika kukabiliana na changamoto hiyo.
‎
‎“Ni ukweli kwamba Mji huu wa Mkuranga unakua kwa kasi, na huduma ya maji haina mbadala, mahitaji yanaongezeka kila siku. Ni lazima wananchi wapate maji. Ununuzi wa pampu hii utaenda kumaliza changamoto ya maji Mkuranga Mjini na kuondoa mgao wa maji,” amesema Mhe Ulega.


‎Hata hivyo, amesema bado kuna baadhi ya maeneo yanayokabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji, ikiwemo Kata ya Mipeko, na kuitaka DAWASA kuweka mipango ya muda mfupi na mrefu ili kuhakikisha changamoto hiyo inatatuliwa.
‎
‎Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire amesema Mamlaka inatambua changamoto ya maji katika Mkuranga na tayari imeanza kuchukua hatua za kuipatia ufumbuzi.


‎
Amesema mapema Oktoba mwaka huu DAWASA itaanza uchimbaji wa kisima kipya cha maji katika eneo hilo ili kuongeza uzalishaji na kusaidiana na kisima kilichopo.
‎
‎Ameongeza kuwa DAWASA pia inapanga kupanua mtandao wa maji katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa na huduma hiyo, ikiwemo Kiguza, Hoyoyo na Mipeko.
‎
‎Kwa mujibu wa Bwire, mpango wa muda mrefu wa Mamlaka ni kutumia vyanzo vya maji vilivyopo Mpera na Kimbiji kusambaza maji hadi Wilaya ya Mkuranga, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa maji kwa wakazi wa maeneo hayo.