Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limesherehekea miaka 95 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1931, likijivunia mafanikio yaliyopatikana katika safari ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini.
Akizungumza katika maadhimisho hayo yaliyofanyika leo katika Ofisi za TANESCO jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, amewashukuru watumishi wa shirika hilo wanaokadiriwa kufikia 13,000 na zaidi kwa kujituma na kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia taratibu na miongozo ya kazi.

Aidha, amewashukuru wateja zaidi ya milioni 6.5 wa TANESCO kwa kuendelea kuiamini taasisi hiyo, akieleza kuwa shirika linatambua umuhimu wa huduma ya umeme katika kuwawezesha wananchi kutekeleza shughuli zao za kila siku.
“Tunawashukuru sana watumishi wote waliopo kwa sasa ambao wanakadiriwa kufikia elfu kumi na tatu na zaidi kwa kazi kubwa ya kuendelea kujitoa na kuhakikisha tunafanya kazi kwa mujibu wa taratibu zetu. Tunashukuru sana wateja wetu zaidi ya milioni 6.5. Tunafahamu wateja wamewekeza hisia nyingi sana kwetu kwa maana ya huduma tunazotoa kuwawezesha kufanya kazi zao za kila siku,” amesema Bw. Twange.

Ameongeza kuwa TANESCO inathamini pongezi na mrejesho chanya kutoka kwa wananchi, wakiwemo watu maarufu na washawishi wa mitandao ya kijamii wanaotambua na kupongeza kazi zinazofanywa na shirika hilo.
Amesisitiza kuwa pongezi hizo ni chachu na dhamana kwa TANESCO kuendelea kuboresha huduma na kutunza imani ambayo wateja wameiweka kwa shirika hilo.

Katika hatua nyingine, Bw. Twange ametoa shukrani kwa Wizara ya Nishati kama wizara mama, Katibu Mkuu wa Wizara, Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya mafuta na gesi, Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO pamoja na wajumbe wengine kwa usimamizi, mwongozo na uwezeshaji wa kibajeti unaoliwezesha shirika kutekeleza majukumu na mipango yake kwa ufanisi.
Amesema ushirikiano na usimamizi huo ni sehemu muhimu ya mafanikio ya TANESCO katika safari yake ya miaka 95, huku shirika likidhamiria kuendelea kuboresha huduma za umeme na kuchangia maendeleo ya Taifa.


