Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
KAMPUNI ya Fuchs, inayojihusisha na uzalishaji wa vilainishi vya injini na mitambo, imekuja na ofa mbalimbali kwa wateja wake kuelekea sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya, ikiwa ni sehemu ya kuwashukuru kwa kuendelea kutumia bidhaa zake.
Mbali na ofa hizo, kampuni hiyo imemtambulisha balozi wake mpya Nana Dolls ambaye atakuwa sehemu ya kampeni za kuitangaza bidhaa za kampuni hiyo pamoja na kuhamasisha matumizi ya vilainishi vinavyoendana na mahitaji ya kila aina ya injini.

Akizungumza wakati wa utambulisho huo, Meneja wa Masoko wa kampuni hiyo Erick Masawe, alisema wameamua kuandaa kampeni hiyo maalumu katika msimu huu wa sikukuu ili kuwapa wateja nafasi ya kunufaika na bidhaa zao kwa bei nafuu na masharti maalumu.
“Tumeandaa ofa mbili ambazo zitahusisha wateja watakaonunua bidhaa zetu pamoja na wale watakaokutana na gari maalumu la kampeni na mhusika atakayekuwa amevalia mavazi ya Father Christmas,”alisema Masawe.

Alifafanua kuwa mteja atakayenunua katoni moja ya vilainishi atapata chupa moja ya ziada bila malipo, huku watakaokutana na gari la kampeni au Father Christmas wakipata fursa ya kununua bidhaa kwa punguzo la nusu bei.
“Katika kipindi hiki cha sikukuu tunataka kurudisha fadhila kwa wateja wetu ambao wamekuwa wakituunga mkono kwa muda mrefu. Tumeandaa ofa mbalimbali ili nao wanufaike na bidhaa zetu,” alisema Masawe.

Alisema Fuchs ni kampuni ya Ujerumani inayojihusisha na uzalishaji wa vilainishi na imefikisha miaka 80 tangu kuanzishwa kwake, huku ikiwa na uzoefu katika kuhudumia sekta mbalimbali zinazohitaji bidhaa hizo.
“Kampuni hiyo imekuwa ikihudumia soko la Tanzania kwa miaka saba, ikitoa bidhaa kwa viwanda mbalimbali vinavyozalisha bidhaa za chakula na sekta ya madini, ambazo zinahitaji vilainishi kwa ajili ya kuendesha mitambo na mashine,”alisema Masawe.

Aliongeza kuwa kuanzia mwakani kampuni hiyo inalenga kuongeza nguvu katika soko la vilainishi vya magari, pikipiki na bajaji, hatua inayolenga kupanua huduma zake kwa watumiaji wa vyombo hivyo vya usafiri.
Masawe alisema moja ya ujumbe muhimu wanaotaka kuwafikishia wateja ni umuhimu wa kutumia vilainishi vinavyoendana na aina na mahitaji ya injini zao.

Alisema kaulimbiu yao ni kuwa kila injini ina mafuta yake, hivyo wamiliki wa magari wanapaswa kupata ushauri sahihi kabla ya kuchagua bidhaa wanayotumia.
“Tunawaambia wateja kuwa kila injini ina mafuta yake. Waje watueleze aina ya gari au injini wanayotumia ili waweze kupata kilainishi kinachokidhi mahitaji yake,” alisema.
Alisema kampuni hiyo itaendelea kuimarisha huduma zake nchini kwa kutoa bidhaa zenye ubora na kuongeza uelewa kwa watumiaji kuhusu matumizi sahihi ya vilainishi, huku akiwakaribisha wateja kutumia fursa ya ofa zilizotangazwa katika kipindi cha sikukuu.


