TAEC YATAKIWA KUSIMAMIA KWA UMAKINI UFADHILI WA ‘SAMIA SCHOLARSHIP’

Na Aziza Masoud,Dar es Salaam 

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda ameitaka bodi mpya ya Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) kusimamia kwa umakini ufadhili wa masomo katika masomo ya elimu ya juu ya teknolojia ya nyuklia, ufadhili uliopewa jina la ‘Samia Scholarship Extended Program’.

Profesa Mkenda ameyasema hayo jana mkoani Dar es Salaam, wakati akizindua bodi mpya ya TAEC, na kusisitiza taasisi hiyo kuzidi kutenga fedha kwa ajili ya ufadhili wa ‘Samia Scholarship Extended Program’ ambao huwawezesha watanzania kusoma nje ya nchi fani mbalimbali zinazohusu mambo ya atomu na nguvu za nyuklia.

“Nawashauri bodi mpya ya TAEC kuimarisha uhusiano wenu na vyuo vikuu vinavyojihusisna na masuala ya sayansi hasa katika utafiti ili kuweza kupata wanafunzi Bora watakaopata ufadhili,”alisema Profesa Mkenda.

Alisema ni muhimu kutengeneza ushirikia huo ili kuweza kupata wanafunzi ambao watasaida kupata watalaam wenye weledi katika fani ya atomu na nguvu za nyuklia.

Naye Mwenyekiti wa bodi ya TAEC Profesa Joseph Msambichaka amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwakumuacha aendelee kushikilia jukumu hilo na kuahidi kuyatekeleza kama inavyopaswa.

“Hii ni heshima kubwa sana kwangu na naahidi nitatekeleza majumu yangu kadri nitakavyoweza,”alisema Profesa Msambichaka.

Alisema katika kipindi chote atakachoendelea kushika nafasi hiyo atatoa ushirikiano kuhakikisha Taasisi hiyo inafanya kazi kwa mujibu WA sheria.

Awali Mkurugenzi TAEC Profesa Najat Mohammed alisema wataendelea kudhibiti na kuhakikisha wanakuwa makini katika matumizi ya atomiki.

Kikao hicho kiliambatana na mafunzo  kwa wajumbe wa  bodi yaliyoanza Februari 17 mpaka 20 yaliyotolewa na Taasisi ya Uongozi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *