Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile amewapongeza wafanyakazi wa Wizara ya Uchukuzi pamoja na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kwa kufanya vizuri katika kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ambayo ni mikubwa na ya kimkakati.
Kihenzile ameyasema hayo leo Machi 21 2025 wakati wa kufungua mkutano wa baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Uchukuzi na taasisi zake uliofanyika mkoani Dodoma, mkutano ambao hufanyika mara moja kila mwaka.

“Yapo mengi mliyoyafanya na sekta hii imebeba miradi mingi ya kimkakati, na kutokana na umadhubuti wenu tumefikia mahali pazuri na ni maeneo yaliyomletea heshima rais wetu kwakweli mnastahili pongezi,” amesema Kihenzile.
Kihenzile amepongeza jitihada zilizofanyika katika uboreshaji wa miundombinu ya bandari iliyosaidia kuongezeka kwa shehena ya mizigo pamoja makusanyo.

Pia amepongeza jitihada za usimamizi wa ujenzi wa miradi ya matenki 15 ya mafuta, ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR, ujenzi na ukarabati wa meli katika Ziwa Viktoria na ZiwaTanganyika pamoja na ujenzi, upanuzi na ukarabati wa viwanja vya ndege.
Awali akizungumza katika mkutano huo Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi na Mwenyekiti wa baraza hilo Profesa Godius Kahyarara amesema wakati Rais Samia anaingia ofisini sekta ya uchukuzi ilikuwa ikichangia dola bilioni 1.2 lakini kwa takwimu za hivi karibuni za benki kuu sekta ya uchukuzi imechangia dola bilioni 3.

Aidha Prof. Kahyarara amesema kuwa maoteo mapya yanaonyesha kwamba ifikapo mwaka 2030 bandari ya Dar Es Salaam itakuwa na uwezo wa kupokea tani milioni 60 za mizigo jambo ambalo litakuwa na ufanisi endapo mtandao wa reli ya umeme utakuwa umekamilika na kusisitiza kuwa serikali inafanyia kazi jambo hilo.
Pamoja na mambo mengine wajumbe katika mkutano huo wamefanya uchaguzi wa kuwapata viongozi ambao ni Katibu na Makamu katibu wa baraza hilo la wafanyakazi.

