Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
RAIS Dk.Samia Suluhu Hassan anatarajia kuzindua bandari kavu ya Kwala iliyopo mkoani Pwani pamoja na kuanza kwa safari za treni ya mizigo ya reli ya kisasa(SGR) kati ya Dar es Salaam na Dodoma.
Akizungumza jijini Dar es Salaa. leo Julai 25, 2025 Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa hafla ya uzinduzi wa Bandari Kavu ya Kwala inayosimamiwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) itakayoongozwa na Dk.Samia itafanyika Julai 31, 2025, Kwala, mkoani Pwani.

“Bandari Kavu ya Kwala, iliyojengwa Vigwaza, kilomita 90 kutoka Dar es Salaam, ina uwezo wa kuhudumia makasha 823 kwa siku (takribani 339,500 kwa mwaka), sawa na asilimia 30 ya makasha yote ya Bandari ya Dar es Salaam hivyo uzinduzi wa bandari hiyo utaendelea kupunguza foleni ya mizigo bandarini.
“Faida zitakazopatikana ni pamoja na Kupunguza msongamano bandarini na barabarani,kuongeza ushindani wa Bandari ya Dar es Salaam, Kupunguza ajali gharama za usafirisaji sambamba na kukuza ajira na biashara katika Mikoa jirani,”alisema Profesa Mbarawa.

Alisema kuwa eneo hilo lilichaguliwa kutokana na jiografia nzuri na ardhi ya serikali isiyo na migogoro
Profesa Mbarawa ametoa wito kwa wananchi na wadau wa usafirishaji kuhudhuria hafla hiyo na kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazotokana na miradi hiyo muhimu kwa maslah ya Taifa
Ameongeza kuwa, treni ya mizigo ya SGR imeanza rasmi kutoa huduma kuanzia tarehe 27 Juni, 2025 baada ya majaribio kufanyika, ambapo imepunguza muda wa kusafirisha Mizigo kutoka masaa 16 hadi masaa 4 kati ya Dar es Salaam na Dodoma na tayari makampuni kama Azania Group na Dangote Cement zimeshanufaika na huduma hiyo.

Amesema Serikali ya awamu ya sita inaendelea kuboresha reli ya zamani (MGR) kwa kupokea mabehewa 50 mapya na 20 yaliyokarabatiwa ili kuongeza uwezo wa kusafirisha mizigo nchini na kukuza uchumi.
Naye Mkurugenzi wa TPA Plasduce Mbosa amesema Mamlaka imejipanga kikamilifu kuhakikisha bandari ya Kwala inatoa huduma bora na za kiwango cha kimataifa
Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa TRC Mha Machibya Shiwa amesema TRC itaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha huduma ya usafiri wa reli inaimarika nchini.
