Durban, Afrika Kusini.
Naibu Waziri Wa Uchukuz Mheshimiwa David Kihenzile, amesema ziara ya mafunzo katika Bandari ya jiji la Durban imempa uzoefu mpana kuhusu namna uwekezaji wa kimkakati unavyoweza kuongeza ufanisi wa bandari.
Akizungumza baada ya kutembelea bandari hiyo yenye takribani gati 58 zinazohudumia mizigo, magari na abiria Naibu Waziri Kihenzile amesema uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya bandari, reli na ushirikishwaji wa sekta binafsi katika uendeshaji umeiwezesha Durban kuwa miongoni mwa bandari zenye ushindani mkubwa barani Afrika.

“Uwekezaji katika miundombinu ya kisasa na kuunganisha bandari na reli kwa ufanisi kumeongeza kasi ya upakiaji na upakuaji wa mizigo na kupunguza muda wa meli kukaa bandarini,” amesema Naibu Waziri Kihenzile.
Naibu Waziri Kihenzile ameongeza kuwa uzoefu huo ni muhimu kwa Tanzania ambayo inaendelea kuboresha miundombinu yake ya usafirishaji, ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), ukarabati wa MGR pamoja na TAZARA, hatua ambazo zinatarajiwa kuongeza ufanisi wa bandari nchini.

Naye Mkuu wa Usimamizi wa Bandari ya Durban Nahodha Rufus Lekala Amesema mkakati wa Serikali ni kutenganisha bandari kulingana na mzigo unaohudumiwa ili kuongeza usalama na Huduma kwa Abiria na mizigo katika Bandari Nchini humo.
Balozi wa Tanzania Nchini Afrika Kusini Mheshimiwa James Bwana amemuhakikishia Naibu Waziri Kihenzile kuwa Ubalozi utaendeleea kutafuta fursa mbalimbali katika Diplomasia ya Uchumi na kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanatimia.




