Na Aziza Masoud,Dar es Salaam
KAMPUNI ya Izze Ride imezindua mfumo mpya wa usafiri mtandaoni ambao unalenga kuleta mapinduzi katika sekta ya usafirishaji pamoja na kuwainua kiuchumi madereva watakaofanya kazi na mfumo huo.
Akizungumza jana Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Izze Ride Fredrick William, alisema ujio wa mfumo huo mpya wa usafiri wa kidijitali unapenga mapinduzi katika sekta ya usafiri pamoja na huduma za kifedha nchini.
Alisema kampuni hiyo itaendesha mfumo huo kwakutumia teknolojia ya kisasa inayochanganya usafiri na huduma za kifedha (fintech) ili kutatua changamoto zinazowakabili Watanzania.
“Watalaam wetu walijifungia kwa muda wa mwaka mmoja ili kutengeneza mfumo huu ambao ni wa kisasa na umekuja kufanya mapinduzi hasa katika kuondoa changamoto ya usafiri kwa njia ya mtandao,”alisema William.

Aliongeza kwa zaidi ya mwaka mmoja, kampuni hiyo imekuwa ikitengeneza na kujaribu mfumo huo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo benki ya CRDB na pamoja na Mamlaka ya Usafiri wa Maji na Ardhini (LATRA) ambao wamechangia katika kuhakikisha huduma hiyo inakidhi mahitaji ya kisheria na kiutendaji.
” Mfumo huo unatarajiwa kuanza kufanya kazi rasmi baada ya majaribio ya kina yaliyolenga kuboresha huduma kwa watumiaji,”alisema William.
Kwa mujibu wa William, lengo kuu la Izze Ride si tu kutoa huduma ya usafiri wa mtandaoni, bali pia kusaidia kutatua changamoto ya ukosefu wa rekodi za kifedha kwa wananchi wengi.
Alisema kupitia mfumo huo, madereva na abiria wataweza kufanya miamala kidijitali ambayo itarekodi mapato yao na kuwawezesha kupata huduma za kifedha kama mikopo kwa urahisi zaidi.
Aidha, kampuni hiyo imeanzisha mpango wa kijamii kwa kushirikiana na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) utakaowawezesha madereva kuchangia mifuko ya hifadhi ya jamii pamoja na kupata bima ya afya. William alisema Izze Ride itachangia sehemu ya fedha kwa madereva watakaoshiriki mpango huo, hatua inayolenga kuboresha ustawi wao wa maisha na usalama wa baadaye.

Aliongeza kampuni hiyo pia imejipanga kurejesha sehemu ya mapato yake kwa wadau kupitia mfumo wa “referral”, ambapo madereva na abiria watapata faida kwa kuwahamasisha wengine kujiunga na huduma hiyo.
Alisisitiza kuwa lengo la Izze Ride ni kujenga mfumo jumuishi unaowanufaisha watumiaji wote huku ukiimarisha uchumi wa kidijitali nchini.
Naye Mkuu wa Kitengo cha huduma za kibenki Kidigitali wa Benki ya CRDB Catherine Rutenge benki hiyo wamekuwa wakishirikiana wadau tofauti wanaolengga kutatua changamoto za kijamii, ambapo baadhi ya miradi hufanywa moja kwa moja na mingine kupitia washirika wenye maono ya kuifikia jamii kwa upana zaidi.
Alieleza kuwa, kama benki kubwa ya Kitanzania, CRDB imejikita kuhakikisha wananchi wanapata fursa ambazo kwa muda mrefu zilikuwa hazipatikani kwa urahisi. Mbali na kutoa huduma za kifedha, benki hiyo pia inaona jukumu lake katika kuchochea ajira kwa vijana pamoja na kuwawezesha wananchi kushiriki katika uchumi kupitia mikopo na huduma za kisasa za kifedha.

Rutenge ameongeza kuwa CRDB itaendelea kuwa mshirika wa kifedha kwa wananchi katika safari ya kukuza uchumi na kuboresha maisha yao.


