UWT KONDOA KUTOA MSAADA KWA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUM KUELEKEA SIKU YA MWANAMKE DUNIANI

Na Asha Mwakyonde, DODOMA

KATIKA kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake kitaifa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT), wa Chama cha Mapinduzi (CCM),Wilaya ya Kondoa Hadija Kilala, amesema jumuiya hiyo imejipanga kuadhimisha siku hiyo kwa vitendo kwa kutoa misaada kwa watoto wenye mahitaji maalum, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha ustawi wa jamii.

Hayo ameyasema leo Machi 4, 2026 katika mahojiano kupitia simu ya kiganjani, Kilala amesema maandalizi yamefanyika baada ya kikao kilichowakutanisha na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum pamoja na wadau mbalimbali, ambapo walikubaliana kuwa licha ya maadhimisho ya kimkoa kufanyika wilayani Kongwa ni muhimu pia kila wilaya kuwa na maadhimisho yake yatakayogusa moja kwa moja jamii.

Amesema kwa upande wa Kondoa, wamebaini changamoto katika Shule ya Msingi Iboni inayohudumia watoto wenye mahitaji maalum, hivyo kuamua kuadhimisha siku hiyo shuleni hapo kwa kutoa msaada wa sare za michezo (traki suti).

“Baadhi ya watoto wana wazazi wenye uwezo wa kununua sare hizo, lakini wengine hawana uwezo. Lengo letu ni kuhakikisha watoto wote wanakuwa katika mwonekano unaofanana ili wale ambao wazazi wao hawana uwezo wasijisikie unyonge,” amesema Kilala.

Ameeleza kuwa wamekusanya michango kutoka kwa wanachama wa UWT na kufanikiwa kupata sare hizo ambazo zinatarajiwa kukabidhiwa Machi 5 katika maadhimisho ya kiwilaya yatakayofanyika shuleni hapo.

Mbali na Shule ya Msingi Iboni, amesema pia watatembelea shule nyingine ya watoto wenye ulemavu ya Serya, ambako watatoa madaftari, kalamu na vitabu mbalimbali kwa ajili ya kusaidia masomo.

Kilala amefafanua kuwa utoaji wa misaada hiyo ni sehemu ya kuonesha mshikamano na kujali makundi yenye uhitaji maalum katika jamii, sambamba na kuenzi mchango wa wanawake katika maendeleo.

Aidha, amesema wamewaelekeza viongozi wa UWT katika kata zote 29 za wilaya hiyo kuandaa na kuadhimisha siku ya mwanamke katika maeneo yao kwa shughuli zitakazogusa jamii moja kwa moja.