Na Asha Mwakyonde, DODOMA
SERIKALI imeendelea kuongeza uwekezaji katika tafiti za kina za madini kwa lengo la kubaini rasilimali mpya na kuongeza mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa taifa, sambamba na kuwawezesha wachimbaji wadogo kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji.
Hayo ameyasema leo Aprili 27,2026 bungeni ,jijini hapa na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde wakati
akiwasilisha Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2026/2027 amesema Wizara kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), imefanikiwa kufanya tafiti za jiofizikia kwa kutumia ndege nyuki katika maeneo ya Geita, Manyara na Lindi, hatua iliyowezesha kubainika kwa taarifa muhimu za kina za jiolojia katika maeneo hayo.
Ameeleza kuwa pamoja na tafiti hizo, utafiti wa kina wa jiofizikia (High Resolution Airborne Geophysical Survey) umefanyika katika maeneo ya leseni za Shirika la Madini la Taifa (STAMICO),kwa mkoani Lindi, ukiwa na lengo la kuongeza uelewa wa rasilimali zilizopo na kufungua fursa mpya za uwekezaji.
Kwa mujibu wa Mavunde, matokeo ya tafiti hizo yameonesha uwezekano mkubwa wa matumizi ya teknolojia ya ndege nyuki katika upatikanaji wa taarifa za kina za jiofizikia, hususan kwa wachimbaji wadogo, jambo litakalorahisisha utafutaji wa madini kwa gharama nafuu na ufanisi zaidi.
Aidha, GST imekamilisha taratibu za kumpata mkandarasi wa kufanya utafiti wa kina katika vitalu viwili vya kimkakati kusini-magharibi mwa nchi vyenye ukubwa wa kilomita za mraba 176,676.45, sawa na asilimia 18 ya eneo lote la nchi. Utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa taarifa za jiofizikia kutoka asilimia 16 ya sasa hadi kufikia asilimia 34.

Kutokana na changamoto ya upungufu wa taarifa hizo katika baadhi ya maeneo, amesema Wizara imeendelea kuhamasisha kampuni binafsi kufanya tafiti za kina katika maeneo yao ya leseni.
“Mfano ni kampuni ya Barrick ambayo imefanya utafiti kwa kutumia helikopta katika maeneo ya Msalala, Nzega, Igunga, Mbogwe na Nyang’hwale ili kubaini maeneo mapya yenye madini,” ameeleza Waziri Mavunde.
Sambamba na hilo, ameeleza kuwa Wizara kupitia GST inaendelea na ujenzi wa Mfumo wa Usimamizi na Usambazaji wa Taarifa za Jiosayansi na Rasilimali za Madini, ambapo hadi Machi 2026 utekelezaji wake umefikia asilimia 45. Kukamilika kwa mfumo huo kunatarajiwa kuboresha upatikanaji na usimamizi wa taarifa za madini nchini.
Katika hatua nyingine, ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo kwa kuwapatia leseni, mafunzo na huduma za kitaalam. Katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, jumla ya leseni 8,878 za uchimbaji mdogo zimetolewa kupitia Tume ya Madini.
Waziri Mavunde amebainisha kuwa STAMICO imeendelea kutoa msaada wa kitaalam kwa wachimbaji hao katika maeneo ya utafiti, uchimbaji, uchenjuaji na utunzaji wa mazingira, ambapo wachimbaji 451 wamepatiwa mafunzo kupitia vituo vya mfano vya Lwamgasa, Katente na Itumbi.
Amesema huduma ya uchorongaji imeendelea kutolewa ambapo jumla ya mita 3,896.59 zimechorongwa kwa ajili ya utafutaji wa dhahabu huku akisema juhudi za kuongeza thamani ya madini zikionekana katika sekta ya chumvi baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kiwanda cha kusafisha chumvi Nangurukuru, wilayani Kilwa.
Katika kurasimisha shughuli za wachimbaji wadogo, amesema Wizara imebaini na kupendekeza maeneo 99 kwa ajili ya ugawaji, huku maeneo mawili tayari yametengwa katika Mbogwe (Msasa) na Lindi (Ntaka Hill) ambapo jumla ya leseni 104 zimetolewa.
Ameeleza kuwa Serikali pia imeendelea kuratibu ushiriki wa wachimbaji wadogo katika majukwaa ya kitaifa na kimataifa kwa lengo la kuwajengea uwezo na kuwatafutia masoko. Kupitia Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji wa Madini (FEMATA) ambapo wachimbaji wadogo 31 walipata fursa ya mafunzo nchini Uturuki mwezi Septemba 2025.
Katika kuwezesha upatikanaji wa mitaji, ameeleza Wizara kupitia Tume ya Madini imesaini hati ya makubaliano na Benki ya CRDB kwa ajili ya utoaji wa mikopo kwa wachimbaji wadogo, ambapo kikundi cha Songwe Gold Family kinatarajiwa kunufaika na mkopo wa shilingi bilioni 50.
Mavunde amezipongeza benki za CRDB, NMB, NBC, Azania na KCB kwa kuendelea kuwaunga mkono wachimbaji wadogo, huku akitoa wito kwa taasisi nyingine za kifedha kuongeza jitihada za kuwakopesha ili kukuza sekta hiyo muhimu.
Hatua hizi zote zinaakisi dhamira ya Serikali ya kuimarisha sekta ya madini kwa kuongeza tafiti, teknolojia na uwezeshaji wa wadau, ili kuchochea ukuaji wa uchumi na ajira nchini.


