TAFICO KUNUFAIKA NA MIRADI MIKUBWA YA KIMKAKATI, SERIKALI KUPANUA UCHUMI WA BULUU

Na Asha Mwakyonde, DODOMA

SERIKALI imeendelea kufungua ukurasa mpya katika sekta ya uvuvi nchini baada ya kuongeza nguvu katika uvuvi wa bahari kuu kupitia uwekezaji mkubwa wa miundombinu, ununuzi wa meli za kisasa pamoja na kuimarisha Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO), hatua inayotarajiwa kuongeza ajira, mapato ya taifa na kunufaisha uchumi wa buluu.

Hayo ameyasema leo Mei 14, 2026 bungeni jijini hapa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dk.Bashiru Ally Kakurwa wakati akiwasilisha bungeni Mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027,
amesema Serikali inaendelea kuliimarisha Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO),kwa kulipatia vitendea kazi vya kisasa na kuendeleza miundombinu ya uvuvi ili kuongeza tija katika sekta hiyo.

Dk.Bashiru amesema Serikali kupitia ufadhili wa Programu ya Maendeleo ya Uchumi na Jamii ya Japan imepokea meli ya kisasa ya uvuvi wa bahari kuu, TAFICO FV.01, ambayo ilizinduliwa rasmi Aprili 25, 2026 na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Amefafanua kuwa ujio wa meli hiyo ni hatua muhimu katika kuongeza uwezo wa Tanzania kuvuna rasilimali za uvuvi katika Ukanda Maalum wa Uchumi wa Bahari (EEZ), huku pia ukitarajiwa kuongeza mchango wa sekta ya uvuvi katika pato la taifa pamoja na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi.

Aidha, Waziri huyo amesema Serikali imekamilisha ukarabati wa gati maalum la kushusha na kupandishia mazao ya uvuvi katika meli (floating jetty), lililopo Ras Mkwavi, ambalo sasa liko tayari kuhudumia shughuli za meli za uvuvi wa bahari kuu na kuongeza ufanisi wa shughuli za TAFICO.

“Kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Serikali imepanga kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo kukamilisha ununuzi wa meli mbili za uvuvi wa bahari kuu, kukamilisha usanifu wa kina na kuanza ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Bagamoyo pamoja na kuendelea kuimarisha ulinzi wa rasilimali za uvuvi,” ameeleza.

Akizungumzia miradi mingine amesema ni pamoja na kutafuta na kupanua masoko ya bidhaa za uvuvi ndani na nje ya nchi, sambamba na kujenga miundombinu ya kuimarisha mnyororo wa thamani kwa mazao ya uvuvi.

Dk. Bashiru ameongeza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo kupitia TAFICO ikiwemo ukarabati wa ghala la kuhifadhi samaki kwa ubaridi, kiwanda cha uchakataji wa mazao ya uvuvi pamoja na uzalishaji wa chakula cha samaki.

Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuongeza vifaa vya kisasa vya uchakataji na uhifadhi wa samaki ili kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi na kuvutia uwekezaji zaidi katika sekta ya uvuvi wa bahari kuu.

Aidha, amesisitiza kuwa Serikali inalenga kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya uvuvi wa kisasa ili kuhakikisha Tanzania inanufaika zaidi na rasilimali zilizopo katika bahari kuu.

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050 inayolenga kuongeza utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia ubia kati ya Serikali na sekta binafsi kwa asilimia 70.