Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
BODI ya Utalii Tanzania (TTB) imempokea bondia mashuhuri kutoka nchini Marekani Terence Crawford ambaye atafanya ziara nchini kwa muda wa wiki moja ambapo pamoja na mambo mengine atatembelea vituo vya utalii zaidi ya vitano vilivyopo Tjanzania Bara na Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 24, 2026 Mkurugenzi Mkuu wa TTB Ephraim Mafuru alisema ziara hiyo ni muendelezo wa kutangaza utalii nchini ambapo kupitia watu maarufu kutoka nchi mbalimbali wanaojulikana duniani.

“Kama jinsi ambavyo mmeshuhudia bodi ya utalii Tanzania imeweza kumkaribisha kwa mara ya kwanza nchini Tanzania mwanamasumbwi nguli kabisa duniani Terence Crawford ameshaingia nchini na tumeandaa ziara yake ya wiki nzima atakuwa nchini Tanzania.
“Nawashukuru kwakuja kumpokea atakuwepo Tanzania kwa muda wa wiki nzima tutampeleka Serengeti , Ngorongoro , Zanzibar,Tarangire, lakini atakutana na viongozi mbalimbali ili tumpige shule ya utalii wa Tanzania na akiondoka akaiongelee mema nchi yetu pendwa ya Tanzania,”alisema Mafuru.

Alisema TTB kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii tukishirikiana na Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo wamejipanga kendeleza zao la utalii wa michezo nchini.
“Tunafanya hivyo makusudi ili kuwatumia watu mashuhuri ambao wanavipaji ,wana ushawishi mkubwa ili kuisemea mema Tanzania lengo likiwa ni moja kuunganisha mazao ya utalii wa michezo ili yaongezee siku za wageni kuja nchini,mbali na utalii wa wanyamapori utalii wa fukwe ,utalii wa mikutano, utalii wa utamaduni ,sasa Wizara ya Maliasili na Utalii imejikita kusaidia utalii wa michezo.

“Kama mlivyoshuhudia tulikuwa na mchezaji bora kabisa aliyewahi kuchezea Manchester United na pia alichezea timu ya Taifa ya Uingereza ameondoka juzi Rio Ferdinand leo tuna Terence Crawford mwanamasumbwi hajawahi kupigwa shindano lolote ,”alisema Mafuru.
Kwa upande wa Crawford alisema alivyopata mwaliko huo alishukuru na kwamba amepata heshima kubwa kuja nchini Tanzania.


