PROFESA KABUDI:BANGI INAONGOZA KUKAMATWA NCHINI

Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam

WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge,Uratibu na Wenye Ulemavu Profesa Palamagamba Kabudi amesema bangi imeendelea kuwa dawa ya kulevya inayokamatwa kwa wingi zaidi nchini ambapo kwa mwaka 2025 jumla ya tani 1,017.26 zilikamtwa.

Profesa Kabudi ametoa kauli hiyo Mei 29,  2026 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa  kuhusu hali ya dawa za kulevya kuanzia mwaka 2025 hadi Mei 29,2026,alisema serikali kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) katika operesheni zake mbalimbali za lupambana na waingizaji na wasambazaji wa dawa za kulevya nchini bangi iliongozwa kukamatwa zaidi nchini.

“Kwa  mwaka 2025, bangi iliendelea kuwa dawa ya kulevya iliyokamatwa kwa kiwango kikubwa zaidi ambapo jumla ya tani 1,017.26, zilikamatwa. Hata hivyo, kiasi kilichokamatwa kilipungua kwa asilimia 55.97 ikilinganishwa na mwaka 2024. Hii ni kutokana na uteketezaji wa mashamba makubwa ya bangi uliofanyika mwaka 2024 na kuimarika kwa udhibiti ikiwemo utoaji elimu kwa jamii inayojihusisha na kilimo cha bangi kuhusu madhara ya kilimo cha zao hilo,”alisema Profesa Kabudi.

Alisema   mbali na bangi jumla ya tani 26.36 za mirungi zilikamatwa ambapo kiasi hicho kiliongezeka kwa asilimia 42.88 ikilinganishwa na mwaka 2024. 

“Ongezeko hili linaashiriakuimarika kwa operesheni za ufuatiliaji na udhibiti hususan katika maeneo ya mipaka na njia zinazotumika kusafirisha dawa hizo,”alisema Profesa Kabudi.

Alisema kwa upande wa dawa za kulevya za viwandani serikali ilifanikiwa kukamata methamphetamine kilogramu 907.18, heroin kilogramu 672.23, cocaine kilogramu 4.89, MDMA gramu 178 na MDA gramu 7.82.

Aidha, kwa mara ya kwanza, mwaka 2025 Serikali ilikamata tani 29.52 za aina mpya ya dawa za kulevya aina ya Kratom itokanayo na mmea unaoitwa mitrogyna speciosa. 

“Kwa upande wa kratom Dawa hii iliingizwa nchini kama mbolea, baada ya uchunguzi ilibainika kuwa ni dawa za kulevya,mafanikio haya yametokana na kazi kubwa iliyofanywa na DCEA kwa kushirikiana na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama katika kudhibiti mitandao na njia za usafirishaji wa dawa za kulevya kupitia Nchi kavu, anga na majini,”alisema Profesa Kabudi.

Alisema pia serikali iliendelea kuimarisha ukaguzi katika vituo vya forodha,vyombo vya usafiri, kampuni za usafirishaji vifurushi na kwenye kampuni zinazojihusisha na biashara ya kemikali bashirifu na dawa tiba zenye asili ya kulevya kwa lengo la kudhibiti uchepushwaji. Kupitia ukaguzi huo.

“Jumla ya tani 31.76 na lita 183.500 za kemikali bashirifu pamoja na kilogramu 2.36 na mililita 160 za dawa tiba zenye asili ya kulevya zilikamatwa.Kwa upande wa makosa ya dawa za kulevya.

“Mwaka 2025, jumla ya mashauri 1,124 yalifunguliwa katika Mahakama mbalimbali nchini pamojana mashauri yaliyokuwa yakiendelea katika Mahakama mbalimbali nchini, mashauri 1,373 yalitolewa hukumu na Jamhuri ilishinda mashauri 1,058,”alisema Profesa Kabudi.

Alisema mali zenye thamani ya zaidi ya Tsh. Bilioni 3.3 zilizohusishwa na makosa ya dawa za kulevya zilitaifishwa.

Awali akiwasilisha taarifa kuhusu hali ya dawa za kulevya nchini Kamishna  Jenerali wa DCEA Aretas Lyimo alisema taarifa ya Dawa za Kulevya ya Dunia ya mwaka 2025 inaangazia tofauti za matumizi ya dawa za kulevya na athari zake kulingana na jinsia.

Alisema taarifa hiyo inaonesha kuwa wanaume wanaotumia dawa za kulevya ni wengi kuliko wanawake, ambapo takribani robo tatu ya watumiaji wa bangi, cocaine na heroin ni wanaume. 

“Hata hivyo, wanawake wako katika hatari ya kupata madharamakubwa zaidi wanapoanza kutumia dawa hizo, hali inayochangiwa na sababu za kibaiolojia,kwa ujumla, wanawake huanza matumizi katika umri mkubwa zaidi

kuliko wanaume, lakini baada ya kuanza huongeza matumizi ya aina mbalimbali za dawa kwa kasi zaidi na huwa katika hatari ya kupata utegemezi au uraibu wa dawa hizo kwa haraka zaidi kuliko wanaume,”alisema Kamishna Lyimo.

Alisema  katika eneo la Amerika Kaskazini,pengo la matumizi ya bangi kati ya wanaume na wanawake linaendelea kupungua ambapo katika maeneo yenye viwango vya juu vya matumizi, jinsia zote mbili sasa zinatumia bangi kwa idadi inayokaribiana.

“Mwaka 2023, upatikanaji wa huduma za matibabu kwa watu wenye uraibu wa dawaza kulevya uliendelea kuwa mdogo zaidi kwa wanawake kuliko kwa wanaume,”alisema Kamishna Lyimo.